Dar es Salaam. Jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe, bado lipo Kitengo cha Uhalifu wa Kifedha(FCU) kwa ajili ya kupitiwa na kukamilisha upelelezi.
Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha linalomkabili Mkondya pekee yake.
Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama hiyo leo, Julai 22, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mkondya ambaye yupo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha, mwenzake John yupo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakama Kuu, lakini pia hana shtaka la kutakatisha fedha.
Amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, kuwa jalada la kesi hiyo bado lipo FCU kwa ajili ya kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo.
Hivyo, kutokana na hali hii tunaomba mahakama yako itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” amesema wakili Kasala.
Hakimu Magutu alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 3, 2025 itakapotajwa.
Hata hivyo, Mkondya hakuletwa mahakamani hapo na kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2024.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 28, 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na tisa ni ya kutakatisha viwanja.
Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo.
Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa mkaguzi wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.
Katika mashtaka tisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es Salaam na akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo, alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.