Kibano chaja madereva walioshusha watalii kwenye magari hifadhini

Arusha/Dar. Madereva walioshusha watalii kwenye magari eneo la Kogatende, katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, ili kushuhudia msafara wa nyumbu, watakabiliwa na mkono wa sheria.

Wakati Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) likisema limeshayabaini magari yote yaliyohusika katika kadhia hiyo na hatua kali zimeanza kuchukuliwa dhidi ya waongoza watalii waliohusika, Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (Tato) kimesema kimeomba kutoka Tanapa majina ya wahusika na kama kuna wanachama wao, bodi itakaa na watawashughulikia kwa mujibu wa taratibu zao.

Tanapa ikizungumzia tukio hilo, ilisema kumekuwa na picha jongefu na za mnato katika mitandao ya kijamii zikionyesha watalii wakiwa wameshuka kutoka kwenye magari katika eneo la Kogatende, kivuko namba nne, ambalo haliruhusiwi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za shirika hilo.

Taarifa hiyo ya Julai 21, 2025, iliyosainiwa na Catherine Mbena, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Kitengo cha Mawasiliano – Tanapa, ilieleza: “Askari wa Tanapa kutoka kikosi cha Kogatende walifika eneo la tukio na kuwaelekeza watalii hao warudi kwenye magari yao.

“ Ifahamike kwamba kitendo cha kushuka kwenye magari kinaharibu utaratibu mzima wa msafara wa wanyama, husababisha uharibifu wa mazingira na pia kuhatarisha usalama wa watalii, kwani msafara huo wa nyumbu huambatana na wanyama wanaokula nyama kama simba, chui na wengine.”

Amesema kwa mujibu wa sheria ya utalii na uhifadhi, wakosaji iwapo ni mtalii hutozwa faini ya Sh100,000, huku mwongoza watalii anaweza kupewa barua ya onyo, kutozwa faini ya Sh100,000 au kufungiwa iwapo ataonekana ni mkosaji wa mara kwa mara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tato, Elirehema Maturo, katika taarifa kwa vyombo vya habari ya Julai 21, amesema:“Tabia hii si tu inahatarisha usalama wa wageni na wanyamapori, bali pia inatishia uadilifu wa mojawapo ya matukio ya kuvutia zaidi.

“Tato inalaani vikali vitendo hivyo na kusisitiza kwamba haviwakilishi maadili ya viwango vya shughuli za safari nchini Tanzania.”

Amesema tabia hiyo inakiuka moja kwa moja kanuni na mwongozo wa maadili na tabia za mwongozaji wa safari wa Tato, uliochapishwa katika lugha tisa ili kuhakikisha inamfikia kila mmoja. Kanuni hizo pia zimewekwa kwenye tovuti ya Tato.

Katika kipindi hiki cha kupokea watalii wengi, amesema wametoa mafunzo kwa waongoza watalii zaidi ya 1,000 nchini, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa, kujenga uwezo na kuimarisha utendaji kazi.

“Kwa hiyo ni jambo la kukatisha tamaa na halikubaliki kushuhudia mienendo ambayo inapuuza juhudi hizi na kutishia sifa ya tasnia yetu. Tunaamini jukumu letu si tu kulinda wanyamapori na mazingira yetu kwa vizazi vijavyo, bali pia kuwaelimisha wageni wetu jinsi ya kupata safari kwa usalama,” amesema.

Tato imetoa wito kwa wadau wote wa utalii kuzingatia kanuni na kuhakikisha Tanzania inasalia kuwa kivutio cha hadhi ya kimataifa.

Akizungumza na Mwananchi, amesema wamewaomba Tanapa majina ya wahusika na kama kuna wanachama wao, bodi itakaa na watawashughulikia kwa mujibu wa taratibu zao.

Amesema wametumia zaidi ya Sh200 milioni kufundisha waongoza watalii zaidi ya 600, mafunzo yaliyofanyika mkoani Arusha, hivyo walitarajia watakuwa mabalozi wazuri wa kuzingatia taratibu.

“Waongoza watalii wanajua taratibu, ikiwamo wageni kutokuruhusiwa kushuka zaidi ya yale maeneo yaliyoainishwa, yakiwamo wanayotumia kupata huduma za kijamii,” amesema na kuongeza:

“Sheria za uhifadhi zitatumika kuwaadhibu. Tunajiuliza walinzi wa hifadhi walikuwa wapi wakati kule tumewanunulia magari mawili aina ya Land Cruiser (Toyota). Tuliamini askari wanapaswa kuwepo eneo lile ili mtu akikiuka taratibu achukuliwe hatua.”

Amesema: “Uzembe unatokea kwenye usimamizi wa sheria. Lile ni eneo dogo; wangekuwapo, ukimuona mtu anakiuka sheria unampiga picha, unatuma na namba ya gari, akifika getini anatozwa faini.”

Mkurugenzi huyo amesema teknolojia imekuwa, hivyo kamera zingefungwa eneo hilo zingesaidia kupunguza vitendo hivyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tato, Wilbard Chambulo, akizungumza na Mwananchi, amesema wanasubiri orodha ya madereva ambao ni wanachama wao ili wachukuliwe hatua za kinidhamu za kichama, ambazo miongoni mwa hizo ni kufutwa uanachama.

Chambulo amesema kuna wakati ilitolewa adhabu ya Dola 50 za Marekani (zaidi ya Sh100,000) kwa makosa hayo, ambayo ilikuwa ndogo kulingana na fedha zilizokwishakulipwa na mtalii, hivyo kuchochea watu kutozingatia sheria.

Amesema anatarajia adhabu itakayotolewa itakuwa zaidi ya hiyo, akipendekeza kufungiwa kutoa huduma kwa miezi kadhaa ili iwe funzo kwa wengine, huku akitaka kuwe na sheria ya kumfikisha mtu mahakamani kwa kosa hilo.

Vilevile amesema kunahitajika usimamizi madhubuti wa kupeleka idadi ya watalii kulingana na udogo wa eneo hilo.

“Eneo ambalo wanyama wanavuka ni padogo mno, lakini kwa bahati mbaya watalii wanaofika pale kuwatazama ni wengi. Nadhani ifike mahali kuwekwe taratibu za kupeleka idadi kadhaa ya watu hata kwa kuwatoza hela zaidi.

“Kwa kufanya hivyo, mbali ya kuendelea kulipatunza, lakini pia pataiingizia nchi fedha,” amesema na kuongeza kuwa mapendekezo hayo walishawahi kuyafikisha serikalini.

Akizungumzia mapendekezo hayo, Catherine kutoka Tanapa amesema: “Ni kweli Tato walishatoa ushauri kuwe na watalii wachache wanaokwenda eneo hilo. Serikali, katika kutekeleza hili, tumeona tutenge maeneo maalumu ambayo watalii wengi wanapenda kwenda na kuyafanya ukanda maalumu, likiwamo hilo la Kogatende.”

Kuhusu kuongeza tozo, amesema hilo ni mpaka sheria ipelekwe bungeni, ipitishwe na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali.