NDOTO ya mshambuliaji wa Simba SC na Taifa Stars, Kibu Dennis kucheza soka la kulipwa Marekani inakaribia kutimia baada ya klabu ya Nashville kumwongezea wiki ya majaribio kutokana na kile kinachoelezwa ni kivutio kwa makocha wa kikosi hicho.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya karibu na mchezaji huyo, Kibu ambaye yuko Marekani tangu mwisho wa mwezi Juni, alikuwa amepewa wiki mbili za awali za kuonyesha uwezo wake.
Hata hivyo, baada ya kipindi hicho kukamilika, uongozi wa Nashville SC inayoshiriki Ligi Kuu Marekani umevutiwa na mwenendo wake na kuamua kumwongeza wiki nyingine ya tathmini ya kiufundi.
“Kibu anapambana kweli kweli,” alisema mmoja wa watu wa karibu na nyota huyo aliyeko jijini Nashville.
“Hapa soka siyo lelemama. Wachezaji wapo wengi, ushindani ni mkubwa. Lakini mpaka kumpa wiki ya tatu, ina maana ana kitu cha ziada.”
Klabu hiyo inayoshika nafasi ya pili kwenye kundi la Mashariki katika Ligi Kuu ya Marekani, imekuwa na mpango wa kuimarisha kikosi chake hasa upande wa winga mwenye kasi na uwezo wa kucheza namba 7 na 11, ambayo Kibu anaweza kucheza kwa ufanisi mkubwa.
Chanzo cha kuaminika kutoka Marekani, kililiambia Mwanaspoti: “Majaribio yanafanyika na kikosi cha pili (reserve team), lakini waamuzi ni benchi kuu la ufundi. Walianza na wachezaji watano, baada ya wiki mbili watatu walikatwa. Kibu na kijana mmoja kutoka Brazil ndio waliobaki na kuongezewa muda kwa sababu walionesha kitu.”
Kwa upande mwingine, taarifa kutoka Simba SC zinaeleza, iwapo Kibu atafaulu majaribio hayo, Nashville SC italazimika kuwasilisha ofa rasmi ya kumnunua mchezaji huyo, ambaye bado ana mkataba na Wekundu wa Msimbazi hadi mwishoni mwa msimu ujao.
Katika mazungumzo ya awali, kocha wa kikosi cha pili cha Nashville, Michael Nsien ambaye ni msaidizi wa kikosi cha kwanza alieleza kuvutiwa na ubora wa Kibu katika kupiga pasi, kasi, pamoja na uwezo wa kumiliki mpira katika presha.
Hiyo ndiyo sababu inayoelezwa kumtazama kwa karibu zaidi.
Mdau wa soka wa Tanzania anayeishi mjini Nashville, Abdallah Karim, ameieleza Mwanaspoti:
“Waafrika wako wachache kwenye kikosi hiki. Kibu ana nafasi nzuri sana. Kama akijituma wiki hii, naamini anaweza kumsajili, hii timu ina uwezo mkubwa kifedha.”