UONGOZI wa Namungo, uko katika mazungumzo ya kupata saini ya aliyekuwa beki wa kati wa Fountain Gate, Jackson Shiga, ukiwa ni mwendelezo wa kusuka upya eneo la kujilinda, baada ya kuondoka kwa Erasto Nyoni na Mrundi Derrick Mukombozi.
Nyota huyo alijiunga na Fountain Gate dirisha dogo la usajili msimu wa 2024-2025, kwa mkataba wa miezi sita, baada ya kuachana na Coastal Union ya Tanga na kwa sasa anatafuta changamoto sehemu nyingine, huku Namungo ikionyesha kumtaka.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman, alisema tayari wameanza maboresho ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao, ingawa taratibu za utambulisho huo zitafuata katika ukurasa rasmi wa timu hiyo, muda wowote kuanzia sasa.
“Mchezaji yeyote ambaye atapendekezwa na benchi la ufundi iwe ni kwa kumsajili au kuachana naye tutazingatia hilo, wapo ambao tumeachana nao ili kupisha sura nyingine ambazo muda wowote tutazitambulisha katika kikosi chetu,” alisema Ally.
Mwanaspoti linatambua licha ya Abdallah Mfuko aliyetokea Kagera Sugar, Hussein Kazi (Simba) na Abdallah Denis ‘Viva’ wa Coastal Union kudaiwa kujiunga na timu hiyo, Shiga ni pendekezo pia lingine ili kuongeza ushindani zaidi msimu ujao.
Nyota wengine wanaodaiwa kujiunga na ‘Wauaji wa Kusini’, ni kiungo, Lucas Kikoti aliyerejea kikosini hapo akitokea Coastal Union na washambuliaji, Heritier Makambo aliyetokea Tabora United, Cyprian Kipenye (Songea United) na Abdulaziz Shahame wa TMA FC.