Kumekucha… Simba yashusha mrithi Tshabalala

NI kama vile mabosi wa Simba sasa wameamua kujibu kwa vitendo baada ya kuwepo kwa kelele nyingi mtandaoni juu ya kushindwa kufanya usajili na badala yake kutoa ‘thank you’ tu kwa waliokuwa nyota wa timu hiyo, kwa kumshusha beki wa kushoto wa kurithi nafasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Tshabalala aliyedumu Msimbazi kwa muda wa miaka 11 ameaga rasmi baada ya kumaliza mkataba na inadaiwa ameshamalizana na Yanga kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano wa 2025-2026, huku pia beki mwingine wa kushoto, Valentin Nouma naye akipewa ‘thank you’ mapema na klabu hiyo.

Hata hivyo, kitu cha kuvutia ni kwamba mabosi wa Simba wanaendelea kufanya mambo yao kimyakimya kwa kuamua kumshukasha beki wa kushoto kutoka Al Hilal ya Sudan, Khadim Diaw ambaye Mwanaspoti liliwataarifu katika toleo la jana, kwa lengo la kumalizana naye.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 26 alitua saa 8 mchana wa jana ili kumalizana na mabosi wa Msimbazi ikiwa ni mapendekezo ya kocha Fadlu Davids ambaye tayari amesharejea kutoka katika mapumziko huko Dubai.

Inadaiwa kuwa, beki huyo raia wa Mauritania ni kati ya wachezaji watano wa kigeni ambao kocha Fadlu amewapendekeza, huku wanne wakielezwa tayari wameshamalizana na mabosi wa klabu hiyo kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo kwa msimu ujao wa mashindano.

Chanzo cha ndani kililiambia Mwanaspoti, ujio wa Diaw kwamba anakuja kukamilisha kusaini mkataba wa miaka miwili, baada ya kila kitu kukubaliana, huku ikielezwa kocha Fadlu kaukubali ujio kwani ni kati ya waliopendekezwa.

Ujio wa Diaw katika  Simba ni kuziba pengo la aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho Mohamed Hussein ‘Tshabalala’  kwenda kujiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili.

“Kila kitu kimekwenda sawa ujio wake ni kuja kusaini mkataba wa miaka miwili, baada ya kuondoka Tshabalala aliyetumika katika timu yetu kwa muda mrefu ni beki mwenye kasi ana uwezo wa kupanda na kushuka,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema kilianza kumfuatilia Diaw katika Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo ikavutiwa na kiwango chake, ambapo alicheza mechi 12 na alikuwa na kadi za njano mbili.

Nje na kuondoka kwa Tshabalala mchezaji mwingine aliyekuwa anacheza nafasi hiyo aliyeachwa na Simba ni Valentin Nouma rai wa Burkina Faso ambaye aliyesajiliwa msimu ulioisha akitokea FC Lupopo ya DR Congo.

Mbali na beki huyo wa kushoto wa kigeni, Simba pia inaelezwa ipo hatua za mwisho kumalizana na kiungo mshambuliaji Lassine Kouma (21) raia wa Mali kutokea klabu ya Stade Malien, ili kuja kumuongezea nguvu Jean Charles Ahoua aliyemaliza kama Mfungaji Bora wa Ligi Kuu akifunga mabao 16 na asisti 10.

“Muda wowote ataingia nchini kuja kukamilisha palipobakia, kwani kwa asilimia 90 mambo yanakwenda sawa, nje na huyo kuna wachezaji tupo katika mazungumzo nao na wengine tumemalizana nao,” kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa mabosi wa Al Hilal ya Sudan nao walikuwa wakipigia hesabu nyota huyo ili ajiunge na timu hiyo iliyokimbiwa na kocha mkuu, Florent Ibenge aliyejiunga na Azma hivi karibuni.