KATIKA kijiji cha Kikuyu, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, kundi la wasichana wachanga limeamua kuvunja mnyororo wa umasikini kwa kuchukua hatua madhubuti za kupanga uzazi, baada ya kushuhudia changamoto zinazotokana na familia zenye watoto wengi na rasilimali haba.
Irene Kawawa (18), ni miongoni mwa mabinti waliothubutu kuamua tofauti. Akiwa mtoto wa sita kati ya kumi waliotokana na mama mmoja, Irene anakumbuka alivyoshawishiwa kuacha shule ili kumpisha mdogo wake. “Mzazi anakwambia feli ili mdogo wako asome. Huwezi kuendelea hata kama una uwezo,” anasimulia kwa uchungu.
Kwa sasa, Irene ametumia elimu aliyoipata kupitia huduma za outreach kutoka taasisi ya Marie Stopes Tanzania (MST) kuamua kutumia njia za uzazi wa mpango. Akiwa na mwenza wake, wameamua kushiriki kilimo na biashara ndogo ndogo huku wakidhamiria kuwa na familia yenye watoto wanne tu.
“Hata kama mwenza wangu anataka wengi, mimi ndiye ninayebeba mimba. Nimeamua kupanga maisha yangu mapema ili nisiingie kwenye mzunguko wa umasikini niliouona nyumbani,” anasema Irene, ambaye pia amewahamasisha rafiki zake watatu kujiunga na huduma hizo.
Taasisi ya Marie Stopes Tanzania imekuwa chachu ya mabadiliko haya kupitia huduma za outreach zinazowafikia wanawake na wasichana walioko maeneo ya mbali ambako elimu ya afya ya uzazi haipatikani kwa urahisi.
Kupitia kliniki hizo za muda, wauguzi wamekuwa wakitoa elimu, ushauri na huduma mbalimbali za uzazi wa mpango kama sindano, vipandikizi na vidonge kulingana na mahitaji ya kila mwanamke.
Jackline Kizozo ni mfano mwingine wa mafanikio. Alianza kutumia uzazi wa mpango mwaka 2018 akiwa na miaka 19 baada ya kupata elimu kutoka kwa wauguzi wa Marie Stopes kwenye zahanati ya Kikuyu. “Niliona siyo busara kuzaa bila mpangilio. Mtoto niliyemzaa nilitaka akue kwanza,” anasema Jackline.
Aliishia darasa la saba kwa sababu ya hali duni ya kifamilia. “Hakukuwa na mtu wa kutusomesha, hakuna shughuli za kipato. Mwenza wangu ni mkulima wa kawaida. Bila uzazi wa mpango ningezaa kila mwaka,” anaeleza.
Kupitia kampeni zinazoendeshwa na taasisi hiyo, wasichana wengi sasa wanaanza kuelewa umuhimu wa kupanga familia, si kwa sababu ya hofu ya mimba zisizotarajiwa pekee, bali kama njia ya kujiwekea mipango ya maisha.
“Ikiwa tutaendelea kuzaa hovyo, tutazidi kuishi kwenye mzunguko wa umasikini. Bora mtoto apishane miaka ili apate elimu, afya bora na malezi ya kueleweka,” anashauri Irene.
Elimu hii inatambuliwa kama nyenzo muhimu katika kupunguza mimba za utotoni, kuongeza fursa kwa wasichana kuendelea na ndoto zao, na kuwezesha familia vijijini kuwa na ustawi.
Marie Stopes Tanzania imeendelea kuwa nguzo ya matumaini kwa wanawake na wasichana wa vijijini. Kupitia huduma zao, wameweza kuleta mabadiliko ya kweli kwa jamii ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikikumbwa na changamoto za uzazi usiopangwa na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi.
Kwa wasichana kama Irene na Jackline, hatua yao ya kuamua kutumia uzazi wa mpango si tu njia ya kujikinga na mimba zisizotarajiwa, bali ni sauti ya matumaini kwa vizazi vijavyo – kuwa wasichana wanaweza kuamua, kupanga na kutimiza ndoto zao.
Irene Kawawa wa kwanza kulia mwenye sweta la pinki, Jackilne Kizozo na mwenzao wote kutoka kijiji cha Kikuyu Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma wakimsikiliza muhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoka Maria Stopes Tanzania (MST) wa kijiji hicho wakati wakipatiwa elimu ya uzazi wa mpango hivi karibuni