Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma leo Juni 22, 2025 itatoa mwelekeo kuhusiana na usikilizwaji shauri la maombi ya Kikatiba, lililofunguliwa na baadhi ya waumini wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church, dhidi ya Serikali.
Shauri hilo la maombi mchanganyiko limefunguliwa na Dinali Mbaga na wenzake 51 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP).
Katika shauri hilo, waombaji hao ambao Kanisa lao lililoko Ubungo Maji Dar es Salaam, limefungwa na lipo chini ya ulinzi wa Polisi, wanapinga kitendo cha Jeshi la Polisi kuwazuia kukusanyika kwa ajili ya kufanya ibada.
Shauri hilo linalosokilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Cyprian Mkeha, Ephery Kisanya na Zahra Maruma, katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kimetajwa kwa mara ya kwanza Ijumaa, Julai 2025.
Mahakama iliipa Serikali siku 10 kuwasilisha majibu ya utetezi wake ambapo iliita kuwasilisha utetezi huo jana Julai 21 na ikapangwa shauri hilo litajwe leo kwa ajili ya amri muhimu.
Katika shauri waombaji hao wanaomba mahakama hiyo itamke kuwa:
Mosi, wana haki ya uhuru wa kuabudu kama ilivyowekwa wazi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyowekwa wazi katika Ibara ya 19(1) na (3).
Mbili, wana haki ya uhuru wa binafsi kama ilivyowekwa chini ya Ibara ya 15(1) na (2)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Tatu, kwamba, kitendo cha Polisi kwa maelekezo na amri za IGP kuwakamata eneo la Ubungo Maji, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, Juni 29, 2025 walipokuwa wamekusanyika kwa amani na utulivu kwa ajili ya ibada, hakukuwa na sababu ya kisheria na kinakiuka haki zao za uhuru wa kuabudu.
Nne, kwamba, askari polisi kwa maelekezo ya IGP kuzuia shughuli zao za ibada, kuwakamata na kuwaweka rumande katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam ni ukiukaji wa haki zao za uhuru wa kuabudu na hivyo ni kinyume cha Katiba.
Tano, kwamba, Polisi kwa maelekezo na amri za IGP hawana mamlaka ya Kikatiba chini ya Ibara ya 19(1) na (2) ya Katiba kuzuia kwa nguvu shughuli zao za kidini waliokusanyika kihalali kwa sala za kidini Juni 29, 2025 eneo la Ubungo Maji
Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura wakiomba usikilizwaji wake ufanyike kwa haraka, huku Wakili wao Peter Kibatala akieleza katika hati hiyo kuwa linagusa haki nyeti ya uhuru wa kuabudu na kwamba itaendelea kuwa hatarini mpaka shauri hilo litakapoamuliwa.
Hata hivyo, wanadai kuwa askari Polisi ambao wamekuwa wakitekeleza maelekezo na amri za IGP, bila amri yoyote ya Mahakama, sababu za kisheria au sababu za kweli zinazoweza kuelezeka, wamekuwa wakiingilia kwa nguvu shughuli zao za kidini,
Wanadai kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikijirudia kila Jumapili ya mwezi Juni na kwamba Juni 29,2025 walipokuwa wamekusanyika kwa amani na utulivu eneo la Ubungo “Maji”, Dar es Salaam, kwa ajili ya kufanya ibada za Jumapili kwa walipovamiwa na askari Polisi.
Wanadai kuwa kwa maelekezo na amri za IGP walifyatuliwa mabomu ya machozi, kupigwa, kukamatwa na kuwekwa rumande katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam, bila sababu yoyote ya kisheria na kwamba
Waombaji hao wanadai kuwa licha ya kuzuia kwa nguvu na askari hapo kufurahia haki zao za uhuru wa kuabudu, hawajawahi kuoneshwa amri yoyote ya Mahakama au amri nyingine ya kisheria inayowapa Polisi haki ya kuingilia haki zao za uhuru wa kuabudu.
Pia wanadai kuwa hawajui kuhusu uwepo wa amri hizo za Mahakama au amri zingine za Kisheria zinazowakataza wao kuhudhuria na kushiriki masuala ya kidini katika kanisa la Glory of Christ Tanzania Church Ubungo “Maji” Dar es Salaam na maeneo mengine.
Hivyo wandai kuwa vitendo hivyo vya maofisa wa mjibu maombi wa pili (IGP) vinakiuka haki zao za Kikatiba zilizowekwa chini ya Ibara ya 19(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, kuhusu uhuru wa kuabudu,
Pia wanadai kuwa vinakiuka Ibara ya 15(1) na (2) ya Katiba hiyo inayoweka haaki ya uhuru binafsi na kupiga marufuku kukamatwa, kuzuiliwa au kunyimwa uhuru kiholela.