Mapigano yalipuka tena DRC Congo

DRC.  Siku mbili tu baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na waasi wa AFC/M23 jijini Doha, Qatar, mapigano mapya yameripotiwa kuzuka tena katika eneo la Kivu Kusini, hali inayozua maswali kuhusu uimara na uhalisia wa makubaliano hayo mapya.

Kwa mujibu wa mashuhuda walioko katika maeneo ya Uvira na Rurambo, milio ya risasi na mizinga imekuwa ikisikika kwa nyakati tofauti tangu usiku wa kuamkia Jumapili, hali iliyowalazimu mamia ya wakazi kuyahama makazi yao na kutafuta hifadhi maeneo ya milimani karibu na mpaka wa Burundi.

“Hatukutegemea kama mapigano yangerudi haraka namna hii. Tulidhani baada ya Doha, hatimaye tungeweza kulala kwa amani,” amesema Aline Mbusa, mama wa watoto watatu mkazi wa Rurambo aliyekimbilia eneo la Lemera.

Makubaliano ya Doha yalilenga kufungua njia ya mazungumzo ya kina, usitishaji wa uhasama, na kuandaa mazingira ya kuwarejesha wakimbizi waliokimbia machafuko ya miezi ya nyuma. Hata hivyo, hali ilivyo sasa inaashiria changamoto kubwa katika utekelezaji wake, hasa kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi madhubuti wa kimataifa katika maeneo ya mapigano.

Wachambuzi wa usalama wa kikanda wameonya kuwa endapo hali hii haitadhibitiwa mapema, inaweza kusababisha kuvunjika kabisa kwa matumaini ya amani na kuibua wimbi jipya la wakimbizi katika eneo la Maziwa Makuu.

Mpaka sasa, hakuna tamko rasmi kutoka kwa Serikali ya Congo wala uongozi wa AFC/M23 kuhusu sababu za kuvunjika kwa hali ya utulivu, huku juhudi za upatanishi zikiendelea kupitia Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika.

Imeandikwa na Mintanga Hunda na mashirika ya habari