Mapya ajali ya ndege ya jeshi iliyoua wanafunzi

Bangladesh. Idadi ya vifo vilivyotokana na ajali ya ndege ya jeshi kamandi ya angta iliyotokea jana Jumatatu Julai 21, 2025 nchini Bangladesh imeongezeka kutoka 19 na kufikia 27.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Shule na chuo cha  Milestone kilichopo Mtaa wa Uttara jijini Dhaka, saa saba mchana wakati wanafunzi wakiwa darasani. Awali idadi iliyotangazwa ilikuwa wanafunzi 16, walimu wawili na rubani mmoja.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AP, idadi hiyo imeongezeka na kufikia 27 ambapo kwa ujumla wengi wao ni wanafunzi.

Ndege hiyo ya mafunzo baada ya kuanguka ilisababisha moto ulioteketeza jengo la ghorofa mbili. Takribani watu 171 waliokolewa wengi wao wakiwa wanafunzi, baadhi wakiwa na majeraha ya moto. Walipelekwa hospitalini kwa kutumia helikopta, magari ya wagonjwa, bajaji, na hata mikononi mwa wazazi na waokoaji.

Kuongezeka kwa idadi kunatokana na wengine kufariki usiku wa kuamkia leo kutokana na majeraha. Hata hivyo takriban watu 78 bado wamelazwa hospitalini wengi wakiwa wanafunzi.

Katika uokoaji wa jana mwalimu Maherin Chowdhury, aliyesaidia kuwaokoa wanafunzi zaidi ya 20, naye alifariki kutokana na majeraha ya moto.

Kwa mujibu wa kamandi ya Anga, ndege hiyo aina ya F-7 BGI ilipata hitilafu ya kiufundi muda mfupi baada ya kuruka saa 7:06 mchana. Rubani, Luteni Mohammed Toukir, alijaribu kuielekeza ndege sehemu isiyo na watu wengi kabla ya kuanguka.

Haijafahamika ikiwa rubani huyo alijirusha kutoka kwenye ndege au alikuwa ndani wakati wa ajali. Wananchi walieleza kuwa shule ilitikisika ghafla na mlipuko mkubwa ulifuata, na kuwalazimu wanafunzi kukimbia kwa hofu.

Serikali ya Bangladesh imetangaza maombolezo leo Jumanne, huku bendera zikipepea nusu mlingoti nchini kote.

Kwingineko imeelezwa hiyo ilikuwa safari ya kwanza ya rubani huyo ya peke yake baada ya kuhitimu mafunzo.

Ajali hii imetokea ikiwa ni mwezi mmoja tangu ndege ya Air India kuanguka juu ya bweni la chuo cha udaktari huko Ahmedabad, India, na kuua watu 241 kati ya 242 waliokuwemo ndani ya ndege, pamoja na 19 waliokuwa ardhini.

Ajali hiyo inatajwa kuwa mbaya zaidi duniani kwa muongo mmoja.