Mataifa saba yakutana Zanzibar kujadili fursa za uvuvi kwa wanawake, vijana

Unguja. Licha ya Zanzibar kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za bahari na pwani, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar imesema inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ugumu wa upatikanaji wa fedha kwa wajasiriamali wadogo hususan wanawake na vijana. 

Wajasiriamali ambao wanakutana na changamoto hizo ni wasio na uwakilishi wa kutosha katika uongozi na mnyororo wa thamani wa uchumi wa buluu.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Julai 22, 2025 na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo na Mafuta Zanzibar, Dk Mwadini Juma Khatib kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Hamad Bakari Hamad wakati akifungua mkutano wa kikanda wa wadau wa sekta ya bahari kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

“Bado tunakabiliwa na changamoto ya kuwafikia wajasiriamali wote hasa wanawake na vijana ambao hawana uwakilishi katika mnyororo wa uchumi wa buluu, kwani wanakosa fedha za kujiendesha kufanya biashara zao,” amesema Bakari.

Amesema, licha ya kukabiliwa na changamoto hizo bado Serikali inaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa buluu kwa kuwekeza na kuboresha miundombinu ya uvuvi na kuongeza thamani katika bidhaa za bahari.

Pia, amesema Serikali inalenga kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi iendane na sera za kikanda za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kusimamia tafiti, ukusanyaji wa takwimu, na usambazaji wa maarifa ili kuimarisha sera na mipango.

Mbali na hilo, amesema wizara hiyo ina mpango wa kuwezesha upatikanaji wa masoko na fedha, hasa kwa wanawake na vijana wajasiriamali.

Ili kufanikisha hayo, Katibu Bakari ametoa wito kwa mashirika mbalimbali duniani kuwekeza hasa kwa vijana na wanawake katika biashara za uvuvi na ubunifu wa baharini kwa kuainisha viwango vya pamoja na mifumo bora ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika kanda.

Amefafanua kuwa, mkutano huo kufanyika kisiwani humo ni fursa muhimu ya kuvumbua na kushirikiana katika kuunda mustakabali wa uchumi wa buluu wa Zanzibar kuwa mfano wa kuigwa kwa kanda na bara kwa ujumla.

Kwa upande wake, Ofisa Miradi Kilimo kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sindi Kasambala amesema kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi haimaanishi kuongeza kipato pekee badala yake inawapatia heshima na ushawishi na fursa za kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

Sindi ameeleza, kuwa kikao hicho kitaangazia zaidi kuimarisha uwezo wa kiuchumi wa wanawake na vijana katika mnyororo wa thamani wa uvuvi kupitia upatikanaji jumuishi wa masoko.

Ofisa Sindi amesema wanawake wanashiriki kwa kiasi kikubwa katika shughuli za uvuvi ikiwemo usindikaji, usambazaji na  biashara lakini  mchango wao hawapati nafasi.

Hivyo, mkutano huo utapanga hatua madhubuti ili kuhakikisha wanawake na vijana wanapata nafasi na kuongoza mabadiliko ya sekta ya uvuvi.

Naye, Komla Prosper Bissi kutoka Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), amesema kwa sasa ni wakati wa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na vijana na wanawake kwa lengo la kufaidika na sekta hiyo.

Pia, amesema, wanahitaji kupewa mwongozo wa namna ya kuitumia sekta ya uvuvi na kuwezeshwa kifedha kwa sababu wengi wao hawana fedha ndio maana wanakwama kujiendesha.