MAKIPA waliomaliza mikataba Singida Black Stars, Metacha Mnata na Hussein Masalanga wapo katika mazungumzo mapya na uongozi wa timu hiyo, kama wanaweza wakaendelea nao msimu ujao.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, zinasema:
“Tunafanya mazungumzo na makipa hao kwa kumshirikisha Kocha Miguel Gamondi, kama tutafikia nao muafaka basi tutawaongezea mikataba.
“Ni makipa wazuri kwa upande wa wazawa na msimu ujao tutakuwa na mechi nyingi za Ligi Kuu, michuano ya CAF na Kombe la FA, hivyo lazima tuwe na kikosi kipana.”
Alipotafutwa Masalanga ili kuthibitisha hilo, alisema: “Kuna mtu anayenisimamia kuhusu ishu za usajili na amenitaarifu kuwepo kwa mazungumzo hayo, pia ameniambia kuna timu Afrika Kusini imeleta ofa, mambo yakikamilika nitakujulisha.
“Lakini kwa sasa nitafurahi sana tukizungumzia kuhusu michuano ya CHAN ambayo niwaombe Watanzania wajitokeze kwa wingi kuja kutusapoti vijana wao, kwangu hii ni mara ya tatu kujumuishwa kwenye kikosi, inanipa moyo na kuendelea kupambana kuona naaminiwa.”
Msimu uliomalizika, Metacha alimaliza na clean sheet saba, huku Masalanga ambaye mzunguko wa kwanza aliichezea Tabora United kwa mkopo, alirejeshwa kikosini hapo kuongeza nguvu kusaidiana na Amas Obasogie raia wa Nigeria.