Mke anusurika kifo kwa kujifanya mfu

Musoma. Jeshi la Polisi mkoani  Mara linamshikilia Jumanne Kibagi mkazi wa kijiji cha Nyarufu wilayani Bunda kwa tuhuma za kumuua mama mkwe wake sambamba na kumjeruhi mke wake kwa kuwakata na panga.

Kibagi anatuhumiwa kumuua mama mkwe wake Kabula Masanja (50) mkazi wa Kijiji cha Chumwi wilayani Musoma na kumjeruhi mke wake Nyageta Alex (21).

Akizungumza leo Julai 22,2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere alikolazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu, Nyangeta amesema  tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Chumwi wilayani Musoma usiku wa Julai 19,2025.

Nyangeta amesema mumewe  alifanya tukio  hilo baada ya kuvamia na kuingia ndani walipokuwa wamelala yeye na mama yake pamoja na mtoto wake mchanga.

“Hadi sasa sijui aliingiaje mle ndani kwani nilishtushwa na maumivu makali sana kwenye kiganja cha mkono wangu wa kulia nikapiga kelele akanikata tena na panga kisogoni akaniambia ninyamaze kabla sijakaa sawa  akanikata kwenye bega la kushoto ikabidi nijifanye nimekufa ili asiendelee kunijeruhi, akanikata tena kwenye bega la kushoto,” amesema.

Ameeleza kuwa wakiwa hawana cha kufanya Kibagi ambaye alimtambua kuwa ni mume wake alihamia upande alikokuwa amelala mama yake na kuanza kumkata kata na panga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Nyangeta amesema kutokana na purukushani zilizokuwa zikiendelea humo ndani mdogo wake aliyekuwa amelala kwenye nyumba nyingine aliamka na kuamua kuja kuona nini kinaendelea, lakini kabla ya kufanya chochote alipigwa na mpini wa jembe na mtuhumiwa kisha kutishia kumchoma na kisu hivyo kuamua kukimbia ili kuomba msaada kwa majirani.

“Baada ya hapo alikimbia kabla majirani hawajafika, mimi  nikapelekwa Hospitali ya Murangi ambapo kulingana na hali ya mama ilivyokuwa ilibidi madaktari waanze na yeye kwanza kisha ndipo wakaja kunipa huduma,  lakini hali yangu ikawa sio nzuri wakanipa rufaa kuja huku,” amesema.

Hata hivyo imeelezwa kuwa mama yake Nyangeta alifariki muda mfupi akiwa anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata na kusababisha kuvuja damu nyingi.

Nyangeta ambaye ana mtoto wa miezi minne hadi sasa hana taarifa juu ya kifo cha mama yake ambapo Mwananchi imemshuhudia akiomba kuongea na mama yake kwa simu, ili amjulie hali baada ya kuambiwa kuwa amepelekwa hospitali ya rufaa ya kanda Bugando kwa matibabu zaidi.

“Mbona nahisi kama mama amefariki, kwa nini hamtaki niongee naye, mpeni simu niongee naye kwa sababu tangu siku ya tukio sijamjulia hali na sijaongea naye,” amelalamika Nyangeta

Akieleza chanzo cha tukio hilo, Nyangeta amesema aliolewa na kuishi na Kibagi kwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini wakiwa wanaishi kama wanandoa alibaini kuwa mume wake anajihusisha na vitendo vya wizi.

“Mwanzoni nilimuuliza anafanya kazi gani akaniambia ni mgambo lakini nilikuwa nashangazwa na tabia yake ya kuondoka nyumbani usiku na kurudi usiku wa manane na kila nilipokuwa nikimuuliza alikuwa mkali sana, kuna muda alikuwa anaondoka amevaa sare za mgambo na wakati mwingine anavaa kawaida,” amesema.

Amesema mara kadhaa mumewe huyo alikuwa akirudi nyumbani akiwa amejeruhiwa na wakati mwingine akiwa mkali sana, jambo ambalo lilimpa hofu mara kadhaa na hata alipokuwa akihoji hakuwa anapata ushirikiano.

“Kuna siku alirudi akiwa na majeraha na alionekana  amepigwa sana alikuwa amevimba nakumbuka aliniambia tu kuwa kumbe mtu unaweza kufa ndani ya dakika chache, lakini nilipotaka kuhoji zaidi alikuwa mkali ikabidi nichemshe maji nimkande mwili,” ameeleza.

Amesema ilibidi aanze kuchunguza ili kubaini mume wake anajishughulisha na nini ndipo alipobaini kuwa amekuwa akijihusisha na vitendo vya wizi ikiwamo kuvunja maduka na kuiba, jambo ambalo lilimpa hofu na kuamua kuondoka na kurudi nyumbani kwao mwezi mmoja uliopita.

Amefafanua kuwa kitendo hicho cha kurudi nyumbani kwao hakikumfurahisha mume wake ambaye alimuomba arejee ili waishi pamoja, lakini alikataa na baada ya jitihada hizo za mume wake kugonga mwamba alianza kupokea vitisho yeye na mama yake ambapo aliwaambia kuwa atawaua kwa kuwakata na mapanga.

“Yeye anaishi Bunda lakini alikuwa akipiga simu mara kwa mara kwangu mimi na kwa mama na hata siku ya tukio mchana alimpigia  mama akamwambia anakuja kijijini kwetu, na mama akamwambia ukija nakupigia yowe kwa sababu umetishia kutuua,” amesema.

Mama mdogo wa Nyangeta, Nyafuru Tungaraza amesema tayari mama huyo amezikwa kijijini Chumwi.

Amesema mchana kabla ya tukio alikuwa na mama huyo ambapo alipigiwa simu na mtuhumiwa akimueleza kuwa anataka kuja kijijini hapo kumchukua mke wake na mtoto wake.

“Nilimsikia akiongea na simu alipomaliza nikamuuliza kulikoni akasema ni mkwe wake anataka kuja lakini amemkatalia kwa sababu tayari alimtishia kumuua, hivyo hana imani na ujio wake na wala hawezi kuruhusu binti yake arudi tena kwa mwanamume huyo,” amesema.

Amesema mama huyo alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini ambapo alikuwa na jeraha kubwa shingoni lililotokana na kukatwa na panga.

“Nadhani lile jeraha la shingoni ndilo lililosababisha kufariki haraka kwani alikuwa anavuja damu sana, lakini pia  kidole cha mkono wa kushoto kilikatika kabisa na alikuwa na majeraha mengine mengi tu mwilini,” ameeleza.

Daktari wa kitengo cha mifupa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dk Shedrack Mfungo amesema kutokana na uchunguzi waliofanya wamebaini Nyangeta kavunjika mifupa mingi kwenye kiganja cha mkono wake wa kulia pamoja na kwenye bega la kushoto.

“Tulimfanyia upasuaji wa awali na sasa tunajiandaa kufanya upasuaji mwingine kwani tumebaini mifupa mingi kwenye kiganja na bega la kushoto imevunjika, hivyo itabidi awekewe vyuma lakini jeraha la kisogoni sio kubwa sana lenyewe litatibiwa kawaida tu,” amesema  Dk Mfungo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara,  Pius Lutumo amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari jeshi hilo linamshikilia mtuhumiwa huyo kwa uchunguzi zaidi.

“Chanzo cha tukio ni mgogoro kati ya Jumanne na Mke wake Nyangeta ambapo mke alidai mume wake anajihusisha na uhalifu hususan wizi hali iliyosababisha mke kukimbilia nyumbani kwao, na mtuhumiwa mkazi wa kijiji cha Nyarufu Bunda aliamua kumfuata mke wake huko kwao Chumwi na kufanya tukio hilo,” amesema.