Na Mwandishi wetu,Mbeya
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Erica E. Yegella, amewataka watumishi ambao wamepata ajira mpya kuhakikisha wakwenda kufanya kazi kwa weledi na maarifa kwa kuzingatia sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Yegella ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wapya wa halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na kuwataka kufanya kazi na kuwaheshimu viongozi wengine kwenye maeneo wanayokwenda wakiwemo viongozi wa dini na wale viongozi wa dini.
Aidha mkurugenzi huyo amewataka kwenda kuwa kioo kwa jamii na wenye kutunza maadili ikiwemo kwenye eneo la mavazi akiwaasa kuzingatia mavazi ya utumishi wa umma hususani wanapokuwa katika utendaji wao.
Erica amesisitiza kufanya kazi kwa bidii na kutokuwa na makundi yasiyo faa kazini na katika jamii kwa ujumla.
Pamoja na maonyo, maelekezo na ushauri wake pia mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Mbeya amewataka kuwa na ushirikiano na wakuu wao wa kazi na viongozi watakaokuwa wakifanya kazi pamoja na jamii inayowazunguka ili kudumisha umoja na kuendeleza shughuli za maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji amehitimisha hafla hiyo fupi na watumishi hao kwa kuwaapisha kiapo cha uadilifu na utii pamoja na kutunza siri za utumishi wa umma.