MABOSI wa Namungo wanaendelea na maboresho ya kikosi hicho na licha ya kuendelea kuzungumza na wachezaji wapya, wamemwongezea mkataba wa mwaka mmoja kipa Jonathan Nahimana raia wa Burundi.
Kigogo mmoja wa Namungo aliliambia Mwanaspoti Nahimana alimaliza mkataba, lakini ripoti ya makocha walioondoka, Juma Mgunda na msaidizi wake, Shadrack Nsajigwa ilipendekeza kumbakiza kipa huyo ambaye msimu uliyoisha alimaliza na cleansheets tano.
“Pamoja na kufanya mazungumzo na wachezaji mbalimbali, lakini tunawaongezea mikataba ambao tulikuwepo nao msimu uliyopita akiwemo kipa Nahimana,” alisema kiongozi huyo na kuongeza;
“Pia mazungumzo yetu na wachezaji kutoka Fountain Gate ambao ni Jackson Shiga na Dickson Ambundo (mabao mawili) yamefikia pazuri, ingawa lolote linaweza likatokea kwani kila timu inahitaji kuboresha kikosi kwa kuchukua wachezaji wazuri.”
Kiongozi huyo alisema mchezaji wa kigeni mpya waliyemalizana naye ni Heriter Makambo aliyekuwa Tabora United msimu uliyoisha, alimaliza na mabao sita na asisti nne.
Wachezaji wengi wanaotajwa huenda wakajiunga na timu hiyo ambao Mwanaspoti liliwaandika ni Hussein Kazi (Simba) na Lucas Kikoti (Coastal Union).