Offen Chikola ni Mwananchi | Mwanaspoti

YANGA kumtangaza kiungo mshambuliaji Offen Chikola aliyesaini miaka miwili ni suala la muda tu, kwani ipo  hatua ya mwisho kukamilisha vitu vilivyokuwa vimesalia.

Yanga imemsajili Chikola akitokea Tabora United na ilizishinda Simba, Azam FC na Namungo ambazo zilikuwa zinawania saini yake, mchezaji huyo msimu uliyoisha alimaliza na mabao saba na asisti mbili.

Chanzo cha ndani kutoka klabu  hiyo ambayo ni bingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo, kilisema:

“Kilichobakia ni mchezaji huyo kumuwekea pesa yake benk, kisha mambo mengine yaendelee.

“Baada ya kumwingizia pesa yake ya usajili muda wowote anaweza akatangazwa kwani kila kitu kipo hatua ya mwisho na mashabiki wajiandae kumpokea mchezaji mpya.”

Chanzo hicho kilisema Yanga mikakati yake ni kuhakikisha kikosi kinakuwa imara, ndiyo maana wanasajiliwa vijana kama Chikola wakifanya vizuri

“Mfano mzuri ni Clement Mzize alipandishwa kutoka kikosi chetu cha vijana na sasa anafanya vizuri anahitajika na timu za ndani na nje na msimu uliyoisha alimaliza na mabao 14 na asisti tano.

Mbali na Chikola kumaliza na mabao hayo, pia aliwahi kuibuka mshindi wa tuzo za mwezi katika mechi dhidi ya Yanga, KMC, Kagera Sugar ilikuwa ugenini, Namungo(nyumbani) na mshindi wa tuzo wa Ligi wa mwezi Novemba.