Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amewataka wawekezaji Zanzibar, kujikita na kubuni mbinu bora zaidi katika uzalishaji wa bidhaa za chakula.
Othman ameyasema hayo leo Julai 22, 2025 alipotembelea na kukagua kiwanda cha uzalishaji wa unga wa ngano na chakula cha mifugo cha Flying Fox Mill kilichopo Finya Mgogoni, jimbo la Gando Mkoa koa wa Kaskazini Pemba.
“Kuna mahitaji makubwa ya chakula cha kisasa cha wanyama wa mifugo wakiwemo kuku na ng’ombe ili kuleta uzalishaji bora wa biashara na chakula,” amesema.
Hata hivyo, Othman licha ya kutoa pongezi kwa wamiliki na wafanyakazi wa kiwanda hicho, kilichoanza uzalishaji wake mapema Juni mwaka huu, akiwataka kudumisha usafi, utunzaji wa mazingira na kuzingatia afya ya mlaji.
Naye mmiliki wa kiwanda hicho, Nassor Ahmed Marhun amesema kwa sasa wanakamilisha taratibu nyingine za kiafya ili kupata daktari mtaalamu wa mifugo na uzalishaji wa chakula chao.
Akitoa maelezo ya kitaalamu, mwendeshaji wa kiwanda hicho, Eric Nyaga amesema kiwanda hicho ambacho kina uwezo wa kuzalisha tani 50 za unga wa ngano na tani 15 za chakula cha mifugo kwa siku, kinatoa bidhaa zenye ubora kwa matumizi ya binadamu na wanyama.
Viongozi mbalimbali wa Serikali na siasa, katika hafla hiyo wamejumuika na Othman aliyeambatana na mke wake Mama Zainab Kombo Shaib, Mratib wa ACT-Wazalendo Kisiwani Pemba, Rashid Ali Abdallah, Mwenyekiti wa Mkoa wa kichama wa Wete Pemba, Juma Khamis Ali na Ofisa Mdhamini Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Ali Suleiman Abeid.