Tangazo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) la tarehe 18 Julai 2025 likibainisha kuwa chuo hicho hakitapokea waombaji wa shahada tisa za elimu ya ualimu limebua hisia tofauti.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, kwa mwaka wa masomo wa 2025/26 chuo kicho hakitapokea maombi ya udahili kwenye shahada za Elimu ya Ualimu katika Sayansi, Saikolojia, Biashara, Sanaa, Sayansi ya Taaluma ya Habari na Mawasiliano, Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii, Malezi na Unasihii, Utawala na Uongozi na Mipango ya Sera na Utawala.
Je, kwa tangazo hilo, ni kweli UDOM kimeacha kabisa kutoa shahada za ualimu? Makala haya yanachambua tafsiri ya tangazo hilo na kuangazia mabadiliko ya msingi katika utolewaji wa shahada za ualimu nchini.
Februari 2024, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yenye dhamana ya kusimamia ubora wa elimu ya juu nchini, ilitoa mwongozo wa uandaaji na utoaji wa shahada za kada ya ualimu. Mwongozo huo unaolenga kukidhi mabadiliko makubwa yaliyofanyika kwa ngazi ya sekondari na msingi, unabainisha mabadiliko makubwa ya mitalaa ya shahada za ualimu.
Kwanza, shahada ya ualimu lazima iwe na masomo mawili ya kufundishia na itolewe kwa muda wa miaka mitatu. Hii ina maana kuwa msisitizo unakuwa zaidi katika kukuza uelewa na umahiri wa maudhui ya masomo mawili ya kufundishia tofauti na msisitizo kwenye elimu ya ualimu.
Kwa mantiki hiyo, mwalimu mmoja anajengwa kuwa na uwezo wa kufundisha masomo mawili kwa wakati mmoja anapokuwa shuleni, hatua inayosaidia kupunguza tatizo la ikama ya walimu nchini.
Pili, muundo wa shahada ya ualimu umerekebishwa kusisitiza maeneo manne makubwa, ambayo ni umahiri katika masomo mawili ya kufundishia, mbinu za kumudu darasa, mbinu za kufundishia na mbinu za kufanya tathmini ya ujifunzaji.
Hii ina maana kuwa mafunzo ya ualimu yanakusudiwa kujenga uwezo zaidi wa ufundishaji darasani na si kuchopeka taaluma nyingine sambamba na ualimu. Ili kulitekeleza hili, mfumo wa mafunzo kwa vitendo umefumuliwa kumjengea mwalimu tarajali ujuzi wa kufundisha.
Ukiangalia mwongozo wa uandaaji na utoaji wa shahada za ualimu uliotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania mwezi Februari 2024, vyuo sasa vitaendesha mafunzo ya vitendo kwa kutumia mfumo unaotumika na taaluma za sayansi ya tiba kwa maana ya kufanya mafunzo kwa vitendo wakati akiendelea na masomo yake darasani chini ya uangalizi wa karibu wa wakufunzi wake chuoni na walimu wazoefu shuleni.
Kwa mfumo wa mafunzo kwa vitendo uliokuwepo, mwalimu tarajali wa mwaka wa kwanza, kwa mfano, angeweza kwenda darasani kufundisha kabla hajamaliza kujifunza nadharia za ujifunzaji na ufundishaji jambo lisilowezekana kwenye taaluma nyingine kama tiba na uhandisi. Mwalimu wa sasa atasimama darasani baada ya mkufunzi wake kumpitisha kwenye mizunguko mitatu ya mafunzo kwa vitendo na kujiridhisha kuwa anaelewa vyema sayansi ya ujifunzaji na anaweza kufundisha kwa umahiri. Mabadiliko haya, kimsingi, yanatafsiri kubwa tatu.
Kwanza, kufuta shahada zinazoandaa walimu wanaobobea zaidi kwenye elimu ya ualimu kuliko masomo ya kufundishia.
Hiki ndicho kilichofanywa na UDOM. Ikumbuke kuwa chuo hiki kilikuja na ubunifu wa kuwa na taaluma za ubobezi katika baadhi ya shahada za elimu ya ualimu ili kumuongezea mwalimu thamani badala ya ualimu pekee.
Kwa mfano, badala ya somo la pili la kufundishia, mwalimu wa shahada ya elimu ya ualimu alisoma taaluma dada nyingine kama unasihi, saikolojia, elimu ya watu wazima, masuala ya sera, utawala na kadhalika.
Changamoto, hata hivyo, mfumo wa mafunzo ya darasani na vitendo ulijikita kumuandaa awe mwalimu kama taaluma mama na kuipa uzito mdogo taaluma dada. Katika mazingira ambayo shule inamtarajia awe mwalimu kamili, ni wazi kuwa taaluma yake nyingine inapoteza umuhimu isipokuwa katika mazingira maalum.
Tafsiri ya pili ya mabadiliko hayo makubwa ni kutambua shahada mbili pekee za ualimu kwa vyuo vikuu vyote vinavyoandaa walimu, yaani Shahada ya Awali ya Ualimu katika Sanaa (BA. Ed) na Shahada ya Awali ya Ualimu katika Sayansi (BSc. Ed).
Hili linathibitishwa na mwongozo wa udahili kwa vyuo vikuu kwa mwaka wa masomo 2025/26 uliotolewa hivi karibuni na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania unaonesha kuwa shahada za elimu ya ualimu hazitapokea wanafunnzi kwa mwaka ujao wa masomo isipokuwa taaluma dada zinazohitajika zaidi katika mazingira ya shule kama vile elimu jumuishi na mahitaji maalumu, elimu ya michezo na mazoezi na elimu ya awali.
Shahada hizi mbili za ualimu katika sayansi na sanaa zinamuandaa mwalimu wa darasani badala ya mwalimu anayebobea kwenye mambo mengi, ambayo wakati mwingine yanamtoa nje ya ualimu wa darasani.
Kadhalika, mwalimu mwenye somo moja anakuwa na wigo finyu wa kufundisha unaozibwa na shahada ya ualimu yenye masomo mawili kwa wakati mmoja. Sharti la sasa la kuwa mkufunzi wa chuo cha ualimu ni uzoefu wa ualimu wa shule. Katika mazingira haya, ni wazi hakuna sababu ya msingi kuweka msisitizo kwenye elimu ya ualimu inayolenga kumuandaa mhitimu atakayekuwa mkufunzi moja kwa moja.
Tafsiri ya tatu ya mabadiliko haya ni fursa kwa vyuo vikuu kuona namna ya kubuni shahada zinazojitegemea kuandaa wataalam wengine wanaoweza kufanya kazi katika mazingira ya shule bila kulazimika kuwa walimu.
Kwa mfano, sera ya elimu na mafunzo ya 2014 (toleo la 2023) ina tamko la kisera kuimarisha unasihi na malezi shuleni. Kwa msingi huo, vyuo vikuu vinaweza kuandaa shahada inayoandaa wataalam wa unasihi na malezi watakaofanya kazi katika mazingira ya shule sambamba na walimu bila kufundisha.
Ndio kusema, tunaweza kuangalia namna ya kuutenganisha ualimu na taaluma nyingine dada ili kuhakikisha kuwa mwalimu anabobea kwenye ualimu wake na taaluma nyingine nazo zinapewa uzito unaostahili kukidhi mahitaji maalum katika shule zetu.
Mwandishi ni mhadhiri wa saikolojia na unasihi Chuo Kikuu cha Dodoma na maoni yake hayawakilishi msimamo wa Chuo Kikuu cha Dodoma.