Dar es Salaam. Baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kubadili ratiba ya vikao vyake vya uteuzi wa watiania wa ubunge na uwakilishi, kimetoa ratiba mpya ya vikao vyote kufanikisha mchakato huo.
CCM ilitangaza mabadiliko ya ratiba hiyo, Julai 19, 2025 kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, huku akitaja sababu ni kuwepo idadi kubwa ya majina ya watiania.
Katika ratiba hiyo mpya, kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili Taifa, ndicho kitakachoanza kukaa Julai 27, tarehe ambayo awali ilipangwa kuanza mchakato wa watiania kujitambulisha kwenye kata na wadi.
Ratiba hiyo mpya imetolewa leo, Jumanne Julai 22, 2025, ikieleza kuwa kikao cha Kamati Kuu kuteua majina ya watiania wasiozidi watatu kwa ubunge, uwakilishi na udiwani ili wakapigiwe kura za maoni, kitafanyika Julai 28.
Baada ya kikao hicho, itafuatia mikutano mikuu maalumu ya mikoa ya UWT kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge wa viti maalumu Bara na wagombea ubunge/uwakilishi wa viti maalumy (Zanzibar) vya mikoa Julai 30, 2025.
Agosti 1, utafanyika Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge/uwakilishi wa viti maalumu vijana kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara asubuhi.
Siku hiyo pia, Mkutano Mkuu Maalumu wa wazazi Taifa, itafanyika kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge/uwakilishi wa viti maalumu kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara, mchana.
Mkutano huo, utafuatiwa na Mkutano Mkuu Maalumu wa UWT Taifa kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge wa viti maalumu vya makundi (Tanzania Bara) na ubunge/uwakilishi viti maalumu (Zanzibar), Agosti 2, 2025.