Sababu wanawake kuumwa zaidi magonjwa ya uti wa mgongo

Moshi. Wakati wagonjwa wenye matatizo ya uti wa mgongo zaidi ya 200 wakifanyiwa upasuaji kila mwaka katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC wanawake wametajwa kuwa miongoni mwa waathirika wakubwa wa tatizo hilo.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa ni ubebaji mimba za kufululiza, shughuli nyingi za kuinama bila kupumzika, kubeba mimba za watoto pacha, mtoto kuwa mkubwa tumboni wakati wa ujauzito na unene uliopitiliza.

Hayo yameelezwa na daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa mifupa na uti wa mgongo wa Hospitali ya KCMC, Dk Honest Massawe wakati wa ufunguzi wa kambi ya matibabu ya kibingwa na bobezi ambayo yanafanyika kwa siku tano  hospitalini hapo kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka nchini India.

Kambi hiyo imelenga kuona wagonjwa zaidi ya 500 wenye matatizo mbalimbali ikiwemo, uti wa mgongo, magonjwa ya mgongo, ubongo na mishipa ya fahamu.

Aidha, Dk Massawe amesema magonjwa hayo yasiyoambukiza yameongezeka kwa kasi hivi karibuni na husababisha vifo vingi kuanzia vijana hadi wazee.

“Kwa siku tunaona wagonjwa  sio chini ya 30 wenye matatizo ya uti wa mgongo, ambapo ni sawa  na watu 4,500 kwa mwaka, na kwa mwaka hapa KCMC tunapasua watu sio chini ya 200 wenye matatizo ya uti wa mgongo,” amesema Dk Massawe.

“Matatizo mengi ambayo tunayaona ni uvimbe kwenye ubongo, uti wa mgongo, diski za uti wa mgongo kuchomoka, pingili za uti wa mgongo kuhama, kuvunjika na kubonyea, nyonga kupondeka na magoti kubonyea,” amesema.

Daktari bingwa bobezi wa upasuaji wa mifupa na uti wa mgongo hospitali ya KCMC, Dk Honest Massawe akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya KCMC wakati wa ufunguzi wa kambi ya madaktari bingwa na bobezi kutoka nchini India kwa kushirikiana na madaktari kutoka hospitali ya KCMC. Picha na Janeth Joseph

Amesema asilimia kubwa ya watu wanaoumwa mgongo ni wanawake  kutokana na kazi wanazofanya za majumbani, huku asilimia chache wakiwa ni  wanaume na kwamba ni  kutokana na aina ya kazi wanazofanya na vitendea kazi wanavyotumia.

“Kuna kazi za kuinama, unene uliopitiliza, ubebaji mimba za kufululiza, mtoto kuwa mkubwa au mtoto kuwa zaidi ya mmoja (pacha) baadaye mtu anapata shida ya mgongo sana,” amesema.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tanlink Medical Tourism Agency, Dk Fyumagwa Hassan amesema uwepo wa kambi hiyo itapunguza gharama ya watu kusafiri nje ya nchi na kuhakikisha Watanzania wanapata huduma nafuu na kwa urahisi.

Aidha, amesema wanategemea kuwaona wagonjwa takriban 500 kwa  siku tano ambazo watakuwa hospitalini hapo na kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wagonjwa wanaojitokeza.

“Dhumuni la kuwepo hapa Tanzania ni kuendesha matibabu ya kibingwa na bobezi kwa magonjwa yanayoathiri kichwa, ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu,” amesema Dk Hassan.

Naye, daktari bingwa bobezi wa upasuaji wa mifupa na uti wa mgongo kutoka nchini India, Dk Abdul Azeem amesema wataendelea kushirikiana na madaktari wa KCMC kuhakikisha wanasaidia wagonjwa kupata huduma hiyo ya upasuaji na wamelenga kufanya upasuaji kwa wagonjwa 20.