Dodoma. Siku chache baada ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kutangaza kusitisha udahili kwa kozi tisa za shahada ya kwanza kwenye elimu ya ualimu kwa mwaka 2025/26, Serikali imesema lengo ni kuongeza umahiri wa walimu wanaozalishwa kwenye chuo hicho.
Programu zilizositishwa ni Shahada ya Elimu ya Ualimu katika Sayansi na Tehama, saikolojia, sayansi, biashara, sanaa, watu wazima na maendeleo ya jamii, utawala na usimamizi, ushauri nasaha, sera na mipango.
Leo Jumanne Julai 22, 2025 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amezungumza na waandishi wa habari akisema idadi ya wanafunzi watakaokwenda kusoma UDOM ipo palepale.
Hata hivyo, amesema kozi ambazo zimefutwa maudhui yatarekebishwa kuwiana kwa kwenda kufundisha masomo watakayokwenda kufundisha kwa kiasi kikubwa kuliko kufundisha ualimu.
Ametoa mfano wa kozi moja ya Shahada ya Elimu ya ualimu katika sayansi na Tehama, ambayo amesema inamaanisha mwanafunzi huyo atasoma masomo mengi ya ualimu na kugusa kidogo katika Sayansi na Tehama.
Amesema tayari UDOM inawasiliana na wanafunzi ambao wameomba udahili katika kozi hizo ambao kwa sasa watachukua shahada ya Sayansi katika ualimu (Science with Education) badala ya elimu ya ualimu katika sayansi na Tehama.
“Maana yake dozi ya sayansi sasa ndio itakuwa kubwa, wanafunzi watatumia muda mwingi kusoma masomo watakayokwenda kuyafundisha huko wanakoenda kuliko njia za kufundisha,” amesema Profesa Mkenda.
Amesema mabadiliko hayo yanafanya kutotumia muda mrefu kumfundisha mwanafunzi kuwa mwalimu bila maudhui na sasa atafundishwa maudhui pamoja na kuwa mwalimu.
Amesema kwa kuwa tayari kuna wanafunzi takribani 1,000 walikuwa wameomba kudahiliwa katika kozi hizo, UDOM itawaeleza kuhusu mabadiliko hayo na wao watafanya uchaguzi iwapo watazitaka kozi mbadala, ama la wataenda katika chaguzi mbili nyingine walizochagua awali.
Katika tangazo hilo, UDOM ilisema haitapokea wanafunzi kwa kozi hizo tisa kwa mwaka wa masomo 2025/26.
“Chuo Kikuu kiko katika mashauriano na mamlaka husika ya udhibiti. Iwapo kutakuwa na mabadiliko au taarifa mpya kuhusiana na tangazo hili mtajulishwa mara moja,” ilieleza sehemu ya tangazo hilo.
Akizungumza na Mwananchi, Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Lughano Kusiluka amesema wanawasiliana na wadau wote ambao watapata maelezo baada ya mashauriano kukamilika.
“Mtu yoyote hatakiwi kupata taharuki, tunashauriana na mdhibiti hivyo wasiwe na hofu tutawapa utaratibu tu,” amesema.
Alipoulizwa sitisho hilo limesababishwa na nini, Profesa Kusiluka alisema ni mapema mno na kutaka watu kuwa na subira.
Hata hivyo, kufuatia tangazo hilo kwenye mtandao wa Instagram wa chuo hicho, baadhi ya wadau wa elimu walitaka watoe maelezo mbadala wake nini kwa kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wameshaomba udahili.
“Chuo kimefanya makosa makubwa ilitakiwa tangazo litoke kabla ya wanafunzi hawajaanza kutuma maombi toka tarehe 15. Na bado TCU guide book 2025/26 hizo kozi bado zipo kwa Udom. Why hawajatoa kwenye system ili zisionekane kabisa,”alihoji mtu aliyejitambulisha kwa jina la Clever _Wenger.
Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa UDOM, Rose Mdami amewataka wasihofie bali wawe na subira kwa kuwa watatoa utaratibu mapema na hakuna atakayekosa programu kwa uhitaji wake.
Hivi karibuni, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa aliwataka wanafunzi wanaomba udahili kuangaliwa kwa umakini na waombaji wa shahada ya kwanza ni programu za vyuo husika.
“Leo (Julai 16) tunafungua awamu ya kwanza ya dirisha la udahili katika mwaka mpya wa masomo itakayodumu kwa siku 26, msisitizo kwa waombaji ni kusoma miongozo na kupata taarifa rasmi kutoka vyuo husika sio kusikia habari za mtaani.
“Unataka kusoma programu fulani hakikisha kwamba inapatikana kwenye hicho chuo unachotaka kusoma, kwa maboresho haya ambayo yamefanyika upo uwezekano kuna programu zimefutwa au kubadilishwa hivyo ni lazima uwe makini,” alisema Profesa Kihampa na kuongeza;
“Soma mwongozo wa TCU pia ingia kwenye tovuti ya chuo au wasiliana na chuo moja kwa moja ili kujua taratibu za kutuma maombi na kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo ili kujiridhisha.