Shauri waumini Kanisa la Gwajima lawekewa pingamizi

Dar es Salaam. Wajibu maombi katika shauri lililofunguliwa na waumini wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, wameweka pingamizi juu ya shauri hilo la kikatiba lililofunguliwa katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dodoma.

Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 16408 limefunguliwa na Dinali Mbaga na wenzake 51 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP).

Waombaji wanapinga kitendo cha Jeshi la Polisi kufunga kanisa hilo lililoko Ubungo Maji, Wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam, na kuwazuia kukusanyika kufanya ibada.

Wajibu maombi wameweka pingamizi la awali wakiiomba Mahakama ilitupilie mbali shauri hilo bila kuwapa waombaji nafasi ya kusikilizwa madai yao ya msingi.

Katika pingamizi hilo, AG na IGP wameibua hoja kwamba waombaji hawakupaswa kufungua shauri la kikatiba kwa kuwa walikuwa na njia mbadala waliyopaswa kuitumia kwanza kutafuta nafuu wanazoziomba.

Wakili wa Serikali, Erigh Rumisha kwa niaba ya wajibu maombi, ameeleza hayo wakati shauri hilo lilipotajwa leo, Julai 22, 2025, kwa njia ya mtandao, kuangalia kama taratibu za ubadilishaji nyaraka za kesi zimeshakamilika.

Rumisha ameieleza mahakama kuwa wameshawasilisha majibu ya utetezi dhidi ya madai, pia wamewasilisha pingamizi la awali.

Wakili wa waombaji, Peter Kibatala, anayeshirikiana na Wakili Gloria Ulomy, amesema ni kweli wamepokea majibu ya wadai na pingamizi la awali.

Mahakama imeelekeza kusikilizwa na kuamua pingamizi hilo kwanza kabla ya shauri la msingi.

Baada ya makubaliano ya pande zote, Mahakama imeamuru pingamizi lisikilizwe kwa njia ya maandishi. Hivyo, wajibu maombi wametakiwa kuwasilisha hoja kuhusu pingamizi ifikapo Julai 29, 2025, na waombaji wawe wamejibu ifikapo Agosti 7, 2025.

Wajibu maombi watawasilisha majibu ya hoja za waombaji Agosti 11, 2025, uamuzi ukipangwa kutolewa Agosti 29, 2025.

Shauri hilo linasikilizwa na jopo la majaji Cyprian Mkeha (kiongozi), Ephery Kisanya na Zahra Maruma wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo, Dar es Salaam.

Waombaji wanaomba mahakama itamke kuwa: Mosi, wana haki ya uhuru wa kuabudu kama ilivyowekwa wazi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, hasa katika Ibara ya 19(1) na (3).

Pili, wana haki ya uhuru wa binafsi kama ilivyowekwa chini ya Ibara ya 15(1) na (2)(a) ya katiba hiyo.

Tatu, kitendo cha polisi, chini ya maelekezo na amri za mjibu maombi wa pili (IGP), kuwakamata eneo la Ubungo Maji, wilayani Ubungo, Dar es Salaam, Jumapili ya Juni 29, 2025, walipokuwa wamekusanyika kwa amani na utulivu kwa ajili ya ibada, hakukuwa na sababu ya kisheria na kinakiuka haki zao za uhuru wa kuabudu.

Nne, kwamba askari polisi, kwa maelekezo ya IGP, kuzuia shughuli zao za ibada, kuwakamata na kuwaweka rumande katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam, ni ukiukaji wa haki zao za uhuru wa kuabudu, hivyo ni kinyume cha Katiba.

Tano, kwamba polisi, chini ya maelekezo na amri za mjibu maombi wa pili, hawana mamlaka ya kikatiba chini ya Ibara ya 19(1) na (2) ya Katiba kuzuia kwa nguvu shughuli za kidini za waombaji waliokusanyika kihalali kwa sala za kidini Juni 29, 2025, eneo la Ubungo Maji, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.

Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura wakiomba usikilizwaji wake ufanyike kwa haraka.

Kibatala ameeleza katika hati hiyo kuwa, usikilizwaji wa shauri hilo ni wa dharura kwa kuwa linagusa haki nyeti ya uhuru wa kuabudu ambayo waombaji wadai imekiukwa kwa matendo ya mjibu maombi wa pili, na itaendelea kuwa hatarini mpaka shauri hilo litakapoamuliwa.

Msingi wa madai ya waombaji ni kuwa Ibara ya 19(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, inatoa haki za uhuru wa kuabudu kwa wananchi.

Wanadai kuwa kwa maelekezo na amri za IGP walifyatuliwa mabomu ya machozi, kupigwa, kukamatwa na kuwekwa rumande katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam, bila sababu yoyote ya kisheria na hawajawahi kuonyeshwa amri yoyote ya Mahakama au amri nyingine ya kisheria inayowapa polisi haki ya kuingilia haki zao za uhuru wa kuabudu.