Dar es Salaam. Wakati matumizi ya nishati safi ya kupikia yakiendelea kupigiwa chapuo katika taasisi zenye watu zaidi ya 100, Kibasila inakuwa shule ya kwanza ya msingi kuanza kutumia umeme kuandaa chakula cha wanafunzi.
Shule hiyo yenye wanafunzi 640 sasa inaachana na kuni ilizokuwa ikitumia awali kuwaandalia wanafunzi chakula cha mchana baada ya kuzinduliwa kwa jiko la kisasa la umeme, ambalo litakuwa likitumika ikiwakilisha shule 50 zilizopo katika mradi wa majaribio kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Tabora na Dodoma.
Jiko hilo limejengwa kwa ushirikiano wa Serikali, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Sustainable Energy Forall ikifadhiliwa na Shirika la UKaid-Modern Energy Cooking Service Program (MECS).
Akizungumza baada ya kuzinduliwa jiko hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kibasila, Halima Rukumbwe amesema kuanza kupika kwa kutumia umeme kutarahisisha utoaji wa huduma na chakula kupikwa kwa wakati tofauti na awali.
“Wakati mwingine mvua iliponyesha kuni zilikuwa zinaloana, chakula hakiivi kwa wakati, wanafunzi wanapoteza muda wa masomo kukisubiri, wakati mwingine kinaungua au kikitoka kina moshi,” amesema Halima.
Mkurugenzi Mkaazi wa WFP nchini, Ronald Tran Ba Huy amesema Tanzania ina zaidi ya wanafunzi milioni 11 wa shule za msingi, hivyo kuingiza suluhisho la nishati safi ya kupikia ni hatua muhimu katika kutekeleza mkakati wa kitaifa ulioanzishwa.
Mwaka 2024 Tanzania ilizindua mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia ambao unalenga kuhakikisha asilimia 80 ya watu wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa ifikapo mwaka 2034.
“Kiwango cha kimataifa kinaonyesha watoto milioni 480 hunufaika na angalau mlo mmoja wa shule kwa siku, tafiti zote zinaonyesha kuwa mlo wa shule huongeza mahudhurio, usajili wa wanafunzi na kupunguza utapiamlo,” amesema.
“Lakini wakati huohuo, shule nyingi hutumia nishati ya kuni au mabaki ya mimea kupikia na shule ni wachangiaji wa pili kwa matumizi ya nishati hiyo baada ya kaya,” amesema.
Amesema wanaamini kuwa shule ni kiini muhimu cha kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia jambo ambalo litapunguza ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Amesema kuzinduliwa kwa jiko linalotumia umeme itasaidia kuhamasisha mkakati wa kitaifa kupeleka nishati safi ya kupikia katika kila shule, hospitali na taasisi za umma nchini.
“Uingereza iko tayari kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika safari yake kuelekea nishati safi ya kupikia kupitia ushirikiano, ubunifu na uwekezaji,” amesema.
Profesa Peter Msofe ambaye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, amesema uzinduzi wa jiko hilo unaendana na ajenda ya kutumia nishati safi iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Ninaamini wanafunzi wa shule hii watakuwa mabalozi wa kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia majumbani kwao na watakapokuwa watu wazima wataendeleza suala hili. Ni vyema sasa kuhakikisha mkakati huu unapelekwa katika shule zote Tanzania,” amesema.
Hili linafanyika wakati ambao taasisi nyingi zenye watu zaidi ya 100 tayari zinatumia gesi asilia katika kupika chakula ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa nishati safi.
Hiyo ni baada ya mtandao wa usambazaji wa gesi asilia nchini umeongezeka kutoka kilomita 102.54 Mwaka 2020/21 hadi kilomita 241.58 Aprili 2025 ambao umewezesha kuunganishwa kwa jumla ya nyumba 1,514, taasisi 13 na viwanda 57.
Pia, zaidi ya vyombo vya moto 15,000 vinatumia gesi asilia (CNG), hivyo kupunguza mahitaji ya petroli na dizeli katika uendeshaji wa vyombo vya moto nchini.