Dar es Salaam. Ufanisi katika utendaji ni miongoni mwa sifa zinazotajwa kuipa benki ya Stanbic Tanzania tuzo ya Benki Bora ya Uwekezaji iliyotolewa na taasisi ya Euromoney kwa mwaka 2025.
Tuzo hiyo ambayo inatambua nafasi wa benki katika kutoa suluhisho za kimkakati hasa kwenye sekta ya uwekezaji zinazounga mkono maendeleo ya taifa, kukuza viwanda vya ndani, na kuchangia ukuaji wa uchumi endelevu.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, amesema imekuja wakati ambao benki hiyo inaendelea kuwa mdau muhimu katika uwezeshaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Amesema kuwa katika kipindi cha mwaka uliopita, Stanbic imeshiriki katika miamala iliyosaidia kupanua uwezo wa viwanda, kusaidia uwekezaji wa taasisi na kukuza mazoea endelevu.
“Tuzo hii si kwa ajili ya kutambulika tu, bali kwa thamani tunayoileta kwa Taifa,” amesema Rwegasira na kuongeza: “Tumefanya kazi na wateja katika sekta ya umma na binafsi kuwezesha miradi inayobadilisha maisha na kukuza uchumi. Utambuzi huu ni ushahidi wa imani ya wateja wetu na uzito tunaoweka kwenye nafasi yetu kama mshirika wa uwekezaji.”

Amesema pamoja na kupatiwa mitaji, mikopo ya muda mrefu, na huduma za ushauri zilizosaidia viwanda vya ndani, kuimarisha uendelevu katika uzalishaji, na kusaidia wawekezaji wa muda mrefu kulinda na kukuza fedha zao.
Naye Mkuu wa Idara ya Uwekezaji na Biashara, Ester Lobore amesema benki hiyo imelenga kwenye miamala inayojenga uwezo na kuleta athari chanya ya muda mrefu.
“Tumesaidia wateja kupanua uzalishaji hadi kusaidia taasisi zinazodhibiti akiba ya taifa kwa siku zijazo, lengo ni kuleta thamani halisi. Tuzo hii inaakisi kazi kubwa isiyoonekana machoni pa wengi—lakini ndiyo inayosukuma ukuaji katika kila ngazi,” amesema.
Mbali na kuchakata uwekezaji, benki ya Stanbic pia imekuwa ikisaidia biashara za ndani kuunganishwa na fursa za kimataifa. Ikiungwa mkono na mtandao na utaalamu wa Standard Bank Group, benki hiyo imewezesha kampuni za Tanzania kufikia masoko ya kikanda, kusimamia fedha za biashara na kujiandaa kwa uhamasishaji wa mitaji ya baadaye.
Katika tuzo hizo Standard Bank Group imeshinda jumla ya tuzo 26 barani Afrika katika Tuzo za Euromoney za 2025. Kundi hilo limetajwa kuwa Benki Bora Afrika, Benki Bora ya Uwekezaji Afrika na Benki Bora kwa makampuni makubwa Afrika, miongoni mwa zingine, zikionesha rekodi imara ya utoaji thamani katika bara hili.
Benki ya Stanbic Tanzania imekuwa ikihudumu nchini kwa zaidi ya miaka 30, ikiunga mkono biashara za ndani, vipaumbele vya serikali, na ujumuishaji wa kifedha.