Taifa Stars imeanza vizuri kwenye mashindano maalumu ya CECAFA ya kujiandaa na Michuano ya CHAN 2024 baada ya kuichapa timu ngumu ya Uganda kwa bao 1-0.
Huu ulikuwa mchezo maalumu wa maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ambao umepigwa kwenye Uwanja wa Black Rhino Karatu Mkoani Arusha.
Awali mashindano hayo yalikuwa yanashirikisha timu za Tanzania, Kenya, Uganda na DR Congo, lakini Kenya na Congo zilijitoa huku Senegal ikipewa nafasi ya kushiriki.
Katika mchezo huo, ambao ulihudhuriwa na mashabiki wengi, Stars ilionekana kucheza soka zuri kipindi cha kwanza na kufanikiwa kujipatia bao la mapema lililowekwa kimiani na Iddi Nado katika dakika ya 13 tu ya mchezo huo.
Kabla ya bao hilo, wachezaji wa Stars walipigiana pasi kutoka langoni kwao na mpira ulimfikia mfungaji ambaye alipiga shuti kali kutoka nje ya eneo la 18 na kumshinda kipa wa Uganda.
Kipindi cha pili, Stars ilirudi na kucheza kwa tahadhari kubwa, huku kocha Hemed Morocco akifanya mabadiliko kadhaa ambayo yaliipa timu hiyo ushindi huo muhimu.
Huu ulikuwa mchezo wa tatu wa Stars wa kujiandaa na CHAN baada ya kucheza mechi nyingine mbili nchini Misri, sasa imebakiza mchezo mmoja dhidi ya Senegal kabla haijarejea jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo dhidi ya Burkina Faso Agosti 2, 2025.