Dar es Salaam. Wamiliki wa mabasi na malori nchini Tanzania wameitaka Serikali kufanya marekebisho ya haraka katika sheria wanazozitaja “za kizamani na kandamizi” ambazo zinawawajibisha kwa makosa yanayofanywa na abiria.
Hoja hii imekuja kufuatia kuwepo kwa sheria zinazowabana watoa huduma hizo za usfirishaji kwa vitendo vinavyofanywa na abiria, ilhali wao wakiwa hawana uwezo wa kuvidhibiti.
Wamiliki wa mabasi kupitia umoja wao, Taboa, wamesema wameanza mazungumzo na maofisa wa Serikali, hasa kutoka Wizara ya Uchukuzi, kwa lengo la kutaka mabadiliko ya sheria ambazo wanadai zimekuwa zikiwabebesha mzigo mkubwa watoa huduma wa usafirishaji bila sababu.
Sheria zinazolalamikiwa ni pamoja na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015 na Sheria ya Uhamiaji.
Wamiliki hao wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu sheria hizo kwa kuwa zinawawajibisha moja kwa moja wao, iwapo abiria atakamatwa akisafirisha vitu haramu kama vile dawa za kulevya, kemikali hatarishi kupitia magari yao.
Kwa mujibu wa sheria ya sasa, mmiliki wa basi anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo chambo chake kutaifishwa, ikiwa bidhaa haramu zitagunduliwa ndani ya gari lake.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti dada la The Citizen, Katibu Mkuu wa Taboa, Joseph Priscus amesema hiyo si haki.
“Wakaguzi (makondakta) hawana mamlaka wala vifaa vya kukagua mizigo ya abiria, lakini wamiliki ndiyo wanaadhibiwa kwa kila kifurushi kilichomo ndani ya basi. Ili kuepuka usumbufu huu, tunapendekeza kuwepo kwa skana (ya kukagua mizigo) katika vituo vya mabasi,” amesema.
Taboa inasisitiza wamiliki wawajibike tu kwa mizigo inayopokelewa rasmi kupitia mfumo wa kuhifadhi mizigo, na siyo kwa mabegi binafsi ya abiria.
“Changamoto hiyo inakuwa kubwa zaidi kwa kuwa mabasi mengi ya masafa marefu hayana vifaa vya ukaguzi au mifumo ya usalama kama CCTV ambayo ingeweza kusaidia kugundua vitu hatarishi. Wamiliki wameongeza kuwa madereva na makondakta si askari wa usalama, wala hawajapewa mafunzo ya namna ya kukabiliana na vitisho vya aina hiyo, lakini bado wanatarajiwa kuwajibika kisheria,” amesema.
Hata hivyo, akitoa ufafanuzi wa sheria hiyo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema chombo kitataifishwa pale itakapothibika kuwa kimesafirisha dawa za kulevya na dereva pamoja na kondakta wanafahamu kuhusu usafirishaji huo, kinyume na hapo abiria mwenye mzigo ndiye atachukuliwa hatua.
“Ikiwa abiria atakutwa na dawa za kulevya kwenye chombo cha usafiri, atachukuliwa yeye hatua halafu kondakta na dereva watakuwa mashahidi, watatoa maelezo yao kuthibitisha kumpakia abiria huyo, hii haitahusisha kutaifishwa kwa chombo.
“Ikitokea ikabainika chombo husika kimesafirisha dawa za kulevya bila uwepo wa abiria basi hatua zitachukuliwa kwa chombo na wasafirishaji, ndiyo maana tunasisitiza wawe makini na madereva na makondakta wanaowaajiri,” amesema.
Licha ya ufafanuzi huo, Riziki Mrema, kondakta wa basi moja la mikoani, amesema: “Wakati mwingine abiria wanapanda basi na bangi au vitu haramu bila sisi kujua. Polisi wakivigundua sisi ndiyo tunatiwa hatiani.”
Kadri wito wa mabadiliko ya sheria unavyozidi kushika kasi, wadau wa usafirishaji wanaiomba Serikali ishirikiane nao kwa karibu ili kuunda sheria zinazolinda usalama bila kuwaumiza watoa huduma.
Hoja hiyo ya Taboa imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo (Tamstoa), Chuki Shabani akisema marekebisho ya sheria hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinamuumiza mmiliki wa chombo ni muhimu.
“Hata sisi ni sehemu ya waliotaka marekebisho hayo, hii haihusishi dawa za kulevya tu, hata wahamiaji haramu, unakuta dereva anabeba mizigo au wahamiaji halafu akikamatwa adhabu inaenda kwa mmiliki, maana ukikamata gari unamuumiza mwenye gari.
Tunachotaka sheria ifanyiwe marekebisho kila mtu abebe mzigo wake, mmiliki awajibike na makosa yanayohusu gari ikiwemo ubovu, lakini inapofika kwenye vile vitu vinavyofanywa na dereva akiwa amebeba bangi, magendo, wahamiaji haramu ashughulikiwe yeye. Ukikamata gari yeye anaenda kutafuta kazi sehemu nyingine inakuwa hasara ya mmiliki,” alisema Shabani.
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) imesema tayari hoja hizo za wasafiorishaji zimewasilishwa kwa Tume ya Haki Jinai, hasa katika kipengele cha usafirishaji wa dawa za kulevya.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Latra, Salum Pazzy amesema licha ya hilo, ukali wa sheria hiyo unalenga kupambana na biashara hiyo haramu.
“Watoa huduma wanapaswa kuhakikisha wafanyakazi wao wamepewa mafunzo ya kutosha kuhusu usimamizi wa mizigo. Sheria haitamlinda mtu anayedai kutokujua,” alisema.
“Hata hivyo, tunaendelea kutoa elimu kwa watoa huduma ili waweze kufanya biashara yao bila kukumbana na changamoto zisizo za lazima.”
Mbali na changamoto hizo za kisheria, wamiliki wa mabasi pia wamelalamikia ucheleweshaji wa kimamlaka unaofanywa na taasisi kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na magari kukamatwa kwa saa kadhaa au hata siku kwa sababu za kiutawala kama ukaguzi wa kodi au nyaraka, hali inayosababisha hasara kubwa kiuchumi na malalamiko kwa abiria.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, wamiliki wa mabasi kupitia Taboa wanajiandaa kuwasilisha mapendekezo rasmi ya marekebisho ya sheria hizo, wakitaka kuwe na mgawanyo wa wazi wa uwajibikaji kati ya mzigo wa abiria na ule wa mtoa huduma.
“Ni lazima kuwe na uwajibikaji wa pamoja. Wamiliki wasibebeshwe mzigo wote wa kisheria kwa vitendo vya kila abiria,” amesema Priscus.
Kutokana na hilo, baadhi ya wamiliki wameanza kutafuta namna ya kujinasua na rungu hilo kwa kuangalia uwekezaji katika teknolojia ya usalama kama mifumo ya CCTV na skana za kisasa kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo.
Vilevile, baadhi wanatoa mafunzo kwa wafanyakazi wao ili waimarishe ukaguzi wa mizigo na kufuatilia tabia za abiria kwa ufanisi zaidi.
“Sekta yetu ni muhimu kwa usafirishaji wa watu na ukuaji wa uchumi, lakini bila sheria za haki na mifumo ya kusaidia, tunahatarisha kudhoofisha moja ya huduma muhimu zaidi kwa umma,” amesema.
Suala jingine linaloibua utata ni kutegemewa kwa madereva na makondakta kuthibitisha uraia na utambulisho wa abiria.
Kwa mujibu wa wamiliki, madereva na makondakta si maofisa uhamiaji na hawana uwezo wala mafunzo ya kufanya kazi hiyo. Hata hivyo, pindi wahamiaji haramu wanapokamatwa ndani ya basi, mmiliki ndiye anayehukumiwa.