LIGI ya kikapu Dar es Salaam kwa wanawake (WBDL), inazidi kuwa tamu na huku ukizubaa tu unapigwa mapema.
Baadhi ya timu zimejikuta haziamini kilichowakuta ikiwa ni mzunguko wa 10 umeanza na zilipoteza michezo yao katika ligi hii inayokua kwa kasi.
DB Lioness ilifungwa na Polisi Stars kwa pointi 58-55, Vijana Queens ikafungwa DB Troncatti pointi 69-66 na Jeshi Stars ikafungwa na JKT Stars kwa pointi 53-52.
Katika mchezo wa Polisi Stars na DB Lioness, Polisi iliingia uwanjani ikiwa imejipanga vyema na Lioness iliyokuwa inajiamini ikijivunia mfungaji wao Taudencia Katumbi, bila kujua Polisi ilikuwa imemwandaa Merina Remmy kumkaba katika robo zote nne.
Udhibiti huo ulimfanya kocha wa timu hiyo Mohamed Yusuph, ampumzishe mara kwa mara kwa lengo la kumtuliza ili ajipange upya, hata hivyo hakubadilika.
Katika mchezo huo, Lioness ilianza kuongoza kwa pointi 13-7, robo ya pili na ya tatu Polisi ikaongoza kwa pointi 20-16, 18-11 na robo ya nne Lioness ikapata pointi 15-13.
Vijana Queens itabidi ijilaumu wenyewe kufungwa na DB Troncatti, kwa pointi 69-66, kutokana na kushindwa kutumia nafasi ya kufunga iliyokoswa na Semeni Abeid dakika ya 6, 8 ya robo ya tatu na dakika saba ya robo ya nne.
Mchezo mwingine uliochezwa katika uwanja huo wa Donbosco Upanga, Ukonga Queens iliishinda Kurasini Divas kwa pointi 63-22 na JKT Stars ikaishinda Jeshi Stars kwa pointi 53-50.