Utafiti wabaini uchafuzi maji ya Ziwa Victoria

Mwanza. Utafiti uliofanywa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) umebaini uchafuzi wa maji ya Ziwa Victoria unaongezeka kutokana na virutubisho vinavyotokana na shughuli za kibinadamu hasa katika miji ya Kisumu, Mwanza, Kampala na Entebbe.

Ziwa Victoria ambalo ni ziwa kubwa kuliko yote barani Afrika na chanzo cha mto White Nile lina wastani wa kina cha mita 80 likizunguka nchi tatu za Tanzania inayolimiliki kwa asilimia 51, Uganda kwa asilimia 43 na Kenya asilimia sita.

Ofisa wa rasilimali ya maji LVBC, Mhandisi Simon Ojwak amesema utafiti huo ulianza Juni 8, 2025 na umehusisha upimaji wa maji katika zaidi ya vituo 44 ndani ya ziwa hilo katika nchi hizo.

“Tulichukua sampuli ambazo zingine tulizipima papo hapo na nyingine tukazipeleka maabara. Taarifa tuliyopata itasaidia kuandaa ripoti ya hali ya bonde la Ziwa Victoria mwaka huu na kutoa mwelekeo wa namna ya kukabiliana na uchafuzi wa maji,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa kwa waandishi wa habari iliyotolewa jijini Mwanza Machi 2025 na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), shughuli za kibinadamu za kilimo, utupaji holela wa taka maji na taka ngumu kutoka viwandani na majumbani, ujenzi wa makazi, shughuli za uvuvi na ufugaji samaki zinazofanyika bila kuzingatia taratibu za utunzaji wa mazingira kwa namna moja au nyingine zinachangia ongezeko la virutubisho kwenye ziwa.

Katika taarifa hiyo iliyokuwa ikielezea changamoto za gugumaji vamizi aina ya Salvinia SPP, ilitaja shughuli nyingine ni hoteli au viwanda vilivyopo kandokando ya ziwa bila kuwa na miundombinu ya kukusanya taka, ukataji miti na uchimbaji madini bila kuzingatia dhana ya maendeleo endelevu na kuvamia eneo tengefu la mita 60 kutoka kwenye kingo za ziwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari  Julai 21, 2025 jijini Mwanza wataalamu na watafiti kutoka nchi za Uganda, Kenya na Tanzania wamesema uchafuzi huo unahatarisha maisha ya viumbe wa majini pamoja na maisha ya watu wanaotegemea maji ya ziwa hilo.

Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Maji, Usafi na Umwagiliaji nchini Kenya, Dk Benjamin Nyshitya amesema kutokana na uchafuzi huo, hata samaki wanakimbilia maeneo ya katikati ya ziwa ambako maji bado ni safi kutafuta mazingira salama ya kuishi, hali inayowafanya wavuvi kupata changamoto kubwa kuwavua.

“Uchafu umeongezeka sana katika maeneo yaliyo karibu na miji mikuu. Hii inaathiri shughuli za uvuvi, usafirishaji pamoja na kuongeza gharama za kusafisha na kutibu maji kwa matumizi ya binadamu kwa kiasi kikubwa,” amesema Dk Nyshitya.

Amesema ili kudhibiti hali hiyo, nchi hizo zinapaswa kudhibiti uchafuzi wa maji unaotokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo.

Kamishna Msaidizi wa Wizara ya Maji na Mazingira nchini Uganda, Dk Obubu Peter amesema mara ya mwisho shughuli ya pamoja la kupima ubora wa maji ilifanyika mwaka 2002, hivyo kulikuwa na umuhimu mkubwa wa mataifa hayo kujua hali ya ubora wa maji kwa sasa.

“Hali ya ziwa si nzuri hasa katika maeneo ya pembezoni mwa miji ambapo shughuli nyingi hufanyika ambazo zinaweza kuwa chanzo cha uchafuzi wa maji. Katika sehemu zenye kina kirefu hali ni afadhali…uwepo wa virutubisho kutoka maeneo ya kilimo unachochea kukua kwa mwani wa kijani, kiashiria cha uchafuzi wa maji,” amesema Dk Obubu.

Amesema kama jumuiya, hatua za haraka zinahitaji kuchukuliwa kwa kuwa hata baadhi ya maeneo mitambo ya kusafisha na kutibu maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, haina uwezo wa kuondoa kemikali zote hatari zinazopatikana sasa katika maji ya ziwa hilo.

Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Maji nchini Tanzania, Monica Jushi amesema juhudi za pamoja za nchi za Afrika Mashariki zinahitajika kwa haraka ili kulinda Bonde la Ziwa Victoria kwa ajili ya kizazi kijacho.

“Tumehusisha mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya tathmini ya hali ya maji. Tumeona maeneo yenye magugu maji yanayozuia shughuli mbalimbali. Ushirikiano huu utasaidia kupanga mipango ya kukabiliana na hatari zilizopo,” amesema Jushi.

Naye, Cosmus Muli, Mshauri wa Kiufundi wa Usimamizi wa Rasilimali za Maji wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), amesema shirika hilo limefadhili mradi huo kwa lengo la kulinda ubora wa maji na mazingira ya Ziwa Victoria.

“Baada ya utafiti huu, tunatarajia nchi za Afrika Mashariki kwa kushirikiana na kamisheni kuangalia changamoto zinazopunguza ubora wa maji na kutafuta suluhu ya pamoja,” amesisitiza.