Mbeya. Wadau wa elimu wakiwamo wazazi na walezi wameshauri kuwapo mpango wa Taifa wa kuwasaidia wanafunzi wanaotoka familia zisizojiweza kufikia ndoto zao kielimu.
Kwani, hata baada ya elimu ya msingi kutolewa bure kwa wanafunzi wote, wapo wenye mahitaji maalumu wanaoishi na walezi au wazazi wasioweza kumudu mahitaji ya shule hasa vifaa.
Hili linasemwa wakati ambao Sh916.7 bilioni zimepangwa kutolewa kama mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2025/2026 ikiwa ni ongezeko kutoka Sh787 bilioni zilizotengwa mwaka 2024/2025 na Sh749.4 bilioni mwaka uliotangulia.
Wakuzungumza leo Julai 22, 2025 wakati wa hafla ya upokeaji mahitaji ya shule kwa wenye uhitaji na wanaoishi mazingira magumu, baadhi ya wazazi na walezi wamesema licha ya juhudi za wadau kuwagusa wasiojiweza ila Serikali inaweza kuangalia njia za kuwafikia wenye kipato duni.
Mmoja wa wazazi, Ambangile Mwanyembe amesema pamoja na kutolewa elimu bure bado zipo familia zenye kipato duni zisizoweza kumudu mahitaji ya wanafunzi, akiomba kuwapo mkakati maalumu kuwafikia wenye uhitaji.
“Kama wanavyofanya kwa elimu ya juu kwa kutoa mikopo, mpango huo unaweza kuwafikia elimu ya msingi ambayo ndio muhimu zaidi kwa maisha ya binadamu katika shughuli za kila siku,” amesema Mwanyembe.
Hiyo ni kwa sababu kuna wazazi na walezi wenye kipato duni kiasi cha kushindwa kumudu mahitaji ya wanafunzi.
“Niombe Serikali kwa dhamira yake ya elimu bure, mikopo au ufadhili uanze kwa shule za msingi ambapo elimu hiyo ndio muhimu zaidi” amesema Mwanyembe.
Mzazi mwingine, Tumaini Mwambene amesema ni vyema isiwe mkopo, bali iwe ni ufadhili.
“Serikali ina mkono mrefu inaweza kuwajua wananchi wake na vipato vyao, hawa watoto wetu wenye uhitaji wasaidiwe wapate haki yao ya elimu,” amesema Tumaini.
Mmoja wa wanafunzi aliyepokea vifaa vya masomo, Najma Shaban wa Shule ya Msingi Chonya amesema msaada huo utasaidia kubadili taaluma kwa kuwa awali alipitia magumu ikiwamo kutoshiriki baadhi ya masomo.
“Niwashukuru wadau kwa namna walivyojitolea kwetu, binafsi sikuwa na madaftari lakini hata chakula hatukuwa na uhakika, kwa hali hii inaweza kunibadilisha kitaaluma” amesema mwanafunzi huyo wa darasa la sita.
Naye Ofisa Elimu Kata ya Iyela jijini Mbeya, Nsajigwa Mwakapala amesema mwanafunzi kukosa mahitaji ya darasani yanamnyima utulivu, lakini kumshusha kitaaluma akiomba wadau kuendelea kujitolea kuwagusa wenye uhitaji.
Mkurugenzi wa Shirika la Child Care and Youth Improvement Tanzania, (CHICAYETA), Abigael Abdalah amesema wamekuwa wakiwafikia wahitaji wengi na idadi imekuwa ikiongezeka akiomba nguvu zaidi kwa wadau wa elimu kuungana kwa pamoja.
Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Mwanjelwa, Singwa Mwenemilao amesema benki hiyo imekuwa karibu na sekta ya elimu na imekuwa kinara katika kuwafikia wengi wanaokwama katika masomo.
“Hivyo basi benki yetu itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kusaidia na kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, tumekuwa tukitoa misaada mbalimbali kuwawezesha wanafunzi kufikia ndoto zao” amesema Singwa.