Wamiliki wa saluni wamtwisha RC Kihongosi zigo la tozo, kodi

Arusha. Baadhi ya wamiliki na wafanyakazi wa saluni za kike na kiume mkoani Arusha wamelalamikia kutozwa kodi na tozo mbalimbali ambazo nyingine wamekuwa hawana uelewa nazo, makadirio ya kodi kuwa makubwa hali inayowafanya kurudi nyuma kiuchumi.

Wengine wameiomba Serikali kuwa kada hiyo itambulike na kupatiwa fursa mbalimbali ikiwemo za mikopo inayotolewa na halmashauri, kwani itawasaidia kukuza vipato vyao.

Wamiliki na wafanyakazi hao wametoa kero hizo leo Jumanne Julai 22, 2025 mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi, aliyewaita ofisini kwake kusikiliza changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mmoja wa wamiliki wa saluni mkoani Arusha,Teddy Mchome,akiwasilisha kwa Mkuu wa Arusha,Kenan Kihongosi, changamoto zinazowakabili kupitia kikao baina yao na Mkuu huyo,leo Jumanne Julai 22,2025.

Mmoja wa wamiliki wa saluni hizo, Teddy Mchome amesema wamekuwa na tozo mbalimbali ambazo wanatozwa kwa kujua na wengine kutokujua na wamekuwa wakidhalilishwa pindi wanapokwenda kudaiwa tozo hizo.

“Tuna utofauti wa utendaji kazi, kuna tozo za kawaida tunazijua lakini wakati mwingine TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) unaongezewa makadirio yanakuwa makubwa tofauti na uwezo wako. Bango ukiweka kidogo unatakiwa ulipie, changamoto ni nyingi tunaomba utatuzi.

“Kwa mfano ofisini kwetu walikuja kueleza wafanyakazi wanatakiwa wapime afya na sikuwa najua kuhusu hilo, wakaniambia hata kama sina habari na hilo siwezi kuwa na wafanyakazi kama hawajapima afya,” amesema.

Baadhi ya wamiliki na wafanyakazi wa saluni za kiume na kike mkoani Arusha,wakiwa nje ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,leo Jumanne Julai 22,2025 katika kikao baina yao na Mkuu huyo,Kenan Kihongosi.

Suala lingine ni kuhusu mambo wanayotakiwa kufanya ikiwemo upimaji afya kwa wafanyakazi na kuwa yeye hakuwa na uelewa kuhusu suala hilo ila ameshalipia ila hadi sasa anazungushwa na wafanyakazi wake hawajapimwa afya, licha ya kuwa ameshafanya malipo aliyoelekezwa na wataalamu.

“Mimi sikuwa najua kuhusu suala la kupima afya kwa wafanyakazi, walikuja nikawaambia naombeni mnipe maelekezo nini cha kufanya wakasema kama hujafanya unatakiwa ufunge ofisi. Nikawaomba utaratibu nikapewa na namba ya malipo nikaomba nikapewa nikalipa na kuchukua fomu kwa ajili ya wafanyakazi kujaza.”

“Lakini nilipolipia kwenye ‘control number’ nimefuatilia fomu ili wafanyakazi wakapime afya ila nimezungushwa, wanakuja kuchukua hela tena wakati hawajanipa fomu, kuna vitu wanatutishia kufunga saluni tunaomba tupewe utaratibu wa masuala kama haya,” amedai.

Naye Amos Mfugale amedai mwishoni mwa mwaka jana alifungua saluni ambapo awali hakuwa amelipia leseni Sh40,000 ambapo alijikuta amefungiwa ofisi yake.

“Nilifungiwa ofisi nikatakiwa kulipia leseni ila nilipolipia nilitozwa faini Sh30,000 ya ufunguo ili niweze kufunguliwa ofisi yangu, kiukweli hili linatuumiza sisi kama wafanyabiashara hasa hiyo faini ya funguo,” amedai.

Naye Pascat Lema ambaye ni mtaalamu wa kupaka wanawake wanja, amesema wamiliki wengi wenye saluni wameanzia chini hivyo wakiwezeshwa mikopo wataweza kukuza mitaji yao.

“Wengi ambao leo ni wamiliki wa saluni walianzia chini, watu wanatamani kumiliki saluni lakini uwezo ni mdogo ndiyo maana wengine wanajikuta wakiishia kufanyia kazi barazani na wengine wakitembea kutafuta wateja,” amesema.

“Asha Mtumwa, mmiliki wa saluni eneo la Stendi ndogo ya daladala amemuomba mkuu huyo wa mkoa kutatua changamoto ya baadhi ya wenzao ambao siyo wamiliki wa saluni ambao husubiri wateja barazani na kusababisha wao kukosa wateja.

Amesema changamoto hiyo ni ya muda mrefu na kuwa wamekuwa wakiziwasilisha Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi wakati wao wanalipa kodi na tozo mbalimbali.

 “Kwa kweli tunataabika sana kiasi ambacho tuna madeni na mikopo mbalimbali ambayo tunashindwa kulipa hadi marejesho, jambo hili siyo geni tunaomba utusaidie kwa hilo,” amesema.

Baada ya maelezo hayo, Kihongosi amesema lengo la kikao hicho ni kujitambulisha kwao ili waweze kumfahamu pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi.

Ameahidi zitatatuliwa huku akipiga marufuku utozaji wa faini ya Sh30,000 ambayo wamekuwa wakitozwa baadhi ya wamiliki wa maduka kwa kushindwa kulipa kodi mbalimbali ikiwemo leseni ya biashara.

Amesema watakaobainika kutoza wafanyabiashara hao faini hizo kutoka Halmashauri ya Jiji la Arusha watachukuliwa hatua za kisheria.

Kuhusu ajira amewataka wamiliki wa saluni mkoani hapa kutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao na kuwataka kuchangamkia fursa za mikopo zinazotolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri ili kukuza mitaji yao.

“Tutafanya kikao na wataalamu na changamoto hizi zitafanyiwa kazi ili kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi katika mazingira rafiki na kuhakikisha kila mmoja analipa kodi,” amesema.