Watanzania wafunguliwa mlango kufanya biashara, kuwekeza Marekani

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Elsie Kanza amesema mwaka 2021 hadi 2024, thamani ya biashara kati ya Tanzania na Marekani imeongezeka kutoka Dola za Marekani 380.2 milioni (Sh988.5 bilioni) hadi Dola 778.1 milioni (Sh2 trilioni).

Amesema mafanikio hayo yamechagizwa na juhudi mbalimbali ikiwemo kuingiwa kwa mkataba wa makubaliano (MoU) uliotiwa saini mwaka 2023 ili kuanzisha mazungumzo ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya sekta binafsi za nchi zote mbili.

Balozi Kanza ameyasema hayo usiku wa jana Jumatatu, Julai 21, 2025  kwenye hafla fupi iliyokutanisha chemba za biashara za nchi hizo, Chemba ya Wafanyabiashara wa Marekani Tanzania (AmCham-TZ) na Chemba ya Wafanyabiashara wa Tanzania Marekani (TACC) huku mgeni rasmi akiwa Meya wa Jiji la Dallas Eric Johnson usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam.

“Mkataba wa Motisha ya Uwekezaji na Shirika la Fedha la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (DFC) ili kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa kampuni za Marekani zenye nia ya kufanya biashara nchini Tanzania.

“Kufunguliwa kwa Ofisi ya Biashara ya Tanzania huko Dallas mwaka 2024 na kuanzishwa kwa TACC mwaka 2024 ili kukuza uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya mataifa yetu mawili, pia vimechagiza ongezeko hilo,” amesema Balozi Kanza.

Ameongeza, Tanzania inaendelea kufanya juhudi zaidi ili kuhakikisha uhusiano wa kibiashara kati yake na Marekani unaimarika zaidi kwa manufaa ya wote.

Aidha, uwepo wa meya huyo unaongeza uhusiano wa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, ambapo anatarajiwa kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na mwenzake wa Dar es Salaam ili kuanzisha uhusiano na jiji hilo huku hatua hiyo itaifanya Dar es Salaam kuwa jiji la kwanza barani Afrika kuanzisha uhusiano wa aina hiyo na Dallas.

Meya huyo ambaye amekuja Tanzania kuimarisha biashara na kuendeleza uhusiano wa kiuchumi ziara yake ni sehemu ya kuangazia fursa mbalimbali za biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kujadili maeneo ya ushirikiano ikiwemo biashara, teknolojia, elimu, utalii na uwekezaji.

Akizungumza Meya Johnson amesema Dallas ambayo ni kitovu cha kibiashara nchini Marekani, ikiwa na Pato la Taifa la zaidi ya Dola 688 bilioni na kuiweka kati ya miji sita tajiri zaidi nchini humo na mojawapo ya eneo lenye uchumi unaokua kwa kasi zaidi.

Amesema watu wengi na kampuni zinahamia Dallas kwa sababu ya mazingira mazuri ya biashara, kodi ndogo na kanuni zisizo kandamizi, miundombinu kama viwanja vya ndege, teknolojia.

“Kutokana na hayo Dallas imejenga uhusiano wa kipekee na Tanzania kupitia chemba za wafanyabiashara. Hivyo nahimiza Watanzania kuchangamkia fursa za biashara na kushirikiana kwa dhati. Watanzania waje kutembelea Dallas na kuendeleza ushirikiano wa kweli unaoleta maendeleo halisi kwa pande zote mbili,” amehimiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri amesema Mamlaka itaendelea kuunga mkono mazingira ya uwekezaji kwa kampuni za Marekani zilizopo Tanzania, hasa zile zinazohusiana na Dallas, Texas.

“Tutaendelea pia kusaidia kampuni za Tanzania zinazotaka kutafuta fursa za biashara nje ya nchi, hasa kupitia mikataba na makubaliano ya ushirikiano,” amesisitiza mkurugenzi huyo.

Akizungumza ongezeko hilo, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Mwinuka Lutengano amesema biashara ya nje ikifanyika kwa tija nchi huongeza pato lake na ukubwa wa fedha za kigeni. Fedha hizo mbali na kukuza uchumi na kuongeza thamani ya sarafu yetu hutuwezesha pia kumudu kununua bidhaa nyingi zaidi kutoka nje.

“Bado tuna fursa kubwa ya kuendelea kudumisha ushirika wenye tija, kujenga uwezo wa wafanyabiashara wetu ili kukidhi vigezo vya kuyafikia masoko ya nje na kuendelea kuwajulisha kuhusu uwepo wa fursa hizi kubwa za kibiashara,” amesema Dk Lutengano.

Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga amesema kiwango cha biashara kuongezeka kunatokana na juhudi za Serikali kuongeza uelewa kwa wawekezaji kuhusu fursa zilizopo Tanzania.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd, Bakari Machumu ambaye pia ni Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya BSM Washauri, amesema kutokana na fursa zilizopo kati ya nchi hizi thamani inapaswa kuongezwa kwakuwa inawezekana kukuza biashara.

“Sio ya kujipiga kifua sana kulingana na fursa zilizopo tulipaswa kuzungumzia biashara ya matrilioni. Jitihada zimewekwa kwa muda mfupi imeongezeka sasa tukiongeza juhudi itakua zaidi,” amesema Machumu.

Amesema kinachopaswa kufanyika ni uthubutu ili kuongeza biashara na Marekani. Uthubutu wa kuona fursa na kujiongeza zaidi ikiwemo Watanzania kwenda kutembelea kujifunza Marekani.