Afrika Kusini. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amemfuta kazi Waziri wa Elimu ya juu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Nobuhle Nkabane baada ya tuhuma dhidi yake za kudanganya Bunge na kuteua watu katika bodi za elimu nje ya utaratibu.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Jumanne, Julai 22, 2025 imesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya Nkabane kushindwa kufika kwenye mikutano muhimu ya Bunge alipotakiwa kutoa maelezo juu ya sakata hilo.
Hatua hiyo inafuatia wakati Rais Ramaphosa akiwa chini ya shinikizo, huku baadhi ya mawaziri wa chama cha (ANC) wakikabiliwa na tuhuma za ufisadi, jambo linalozua migogoro ndani ya Serikali ya mseto inayoundwa na vyama kumi.
Ikumbukwe chama kikuu cha upinzani, Democratic Alliance (DA), ambacho sasa ni mshirika katika serikali ya umoja, kiliwasilisha mashtaka dhidi ya Nkabane kwa kulidanganya Bunge.
Taarifa iiyochapiswa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo TRT World, Daily Sun, zinasema waziri mpya ameshachaguliwa.
Hata hivyo, Chama cha DA kimefurahishwa na uamuzi huo wa kutimuliwa kwa Waziri Nkabane ambapo kupitia msemaji wake, Karabo Khakhau, kimesema kuondolewa waziri huyo ni ushindi kwa taifa la Afrika Kusini, hasa katika kupambana na kile walichokiita ufisadi wa watumishi wa ANC.
“Hatuwezi kuwa na mawaziri wenye tuhuma za ufisadi na wanaodanganya Bunge, huku wakiwa na dhamana ya kusimamia fedha za mamilioni ya wananchi wa Afrika Kusini,” amesema Khakhau akinukuliwa na SABC News.
Waziri mwingine achaguliwa
Aidha, kwa mujibu wa SABC, Rais Ramaphosa amemteua Buti Manamela kuwa Waziri mpya na Nomusa Dube-Ncube kuwa Naibu wake.
Hatua ya kumteua Manamela, ambaye hapo awali alikuwa Naibu Waziri katika wizara hiyo, inaelezwa kuwa ni jitihada za Ramaphosa kurejesha imani kwa umma na kudhibiti mvutano wa kisiasa unaoendelea ndani ya serikali ya mseto.