Williamu atamba kushika nafasi ya kwanza

Wakati mchuano mkali wa ufungaji ukiendelea katika Ligi ya kikapu Dar es Salaam (BDL) kwa upande wachezaji wazawa,  Isaya Williamu wa DB Oratory ndiye mchezaji pekee  anayechuana vikali na wa kigeni.

Mchezaji huyo anayecheza nafasi ya namba 2 ‘Shooting Guard’ anashika nafasi ya pili  kwa kufunga pointi 201,  huku ya kwanza ikishikwa na Mkongo Ntibonela Bukeng wa Savio aliyefunga 244.

Mchezaji huyo mwenye kiwango cha juu kwa sasa, amewazidi baadhi ya wachezaji wa kigeni    Junior Louissi kutoka Gabon, Jamel Marbuary (Marekani) na Sharom Ikedigwe (Nigeria),

Louisisi anayeichezea Srelio anashika nafasi nne kwa pointi 144, Marbuary (Dar City) nafasi ya tano kwa pointi 145, huku Ikedigwe akishika ya 10 kwa pointi 133.

Mbali ya kushika nafasi ya pili kwa ufungaji, anashika nafasi ya sita kwa kufunga  eneo moja la three, point 18,  akifuatiwa  na Hassan Kabanda wa Uganda anayechezea pia DB Oratory,  aliyefunga naye ‘three point’ 18.

Williamu aliliambia Mwanaspoti amejipanga kupambana na wachezaji wa kigeni, kwa ufungaji  mpaka ligi hiyo itakapomalizika..

“Hata ukiangalia wachezaji wa kigeni niliowashinda, wana  uwezo mkubwa, kwa kweli  itakuwa ni jambo la kushangaza nisishike nafasi ya kwanza,” alisema Williamu.