Wimbi la vifo vya wanafunzi vyuoni latisha

Dar es Salaam. Katika siku za hivi karibuni, matukio kadhaa ya wanafunzi kujinyonga yameripotiwa katika vyuo mbalimbali nchini.

Mfano wa matukio hayo ni  lile la mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Emmaus Kajura, aliyeripotiwa kujiua Juni 25, 2025, huku Jeshi la Polisi likieleza kuwa linachunguza tukio hilo.

Tukio jingine la kusikitisha lililotokea Juni 17, mwaka huu Chuo cha Sayansi Teknolojia (MUST) Gerald Said (22), mwanafunzi wa mwaka wa tatu aliyefariki dunia baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali tumboni, akidaiwa kushambuliwa na mwanafunzi mwenzake, Emila Joseph, (21) wa mwaka wa kwanza. 

Tukio jingine lililoshtua ni la Erick Sawe, mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kilimanjaro (KICHAS), aliyekutwa amejinyonga Mei 15, mwaka huu, kwa madai ya kuzidiwa na madeni kutoka kwa wanafunzi wenzake.

Mbali na hayo, migogoro ya kimapenzi na visasi miongoni mwa wanachuo, vinatajwa kuwa sababu za  vifo vya wanafunzi wawili katika mikoa ya Iringa na Arusha, jambo linaloashiria kuwapo kwa changamoto kubwa sio tu kwa afya ya akili kwa wanafunzi, lakini pia hofu ya usalama na ustawi duni wa kijamii ndani ya mazingira ya vyuo.

Mlezi wa wanafunzi katika  chuo kikuu kimoja nchini, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, anakiri  ofisi yake kupokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi, yakiwemo ya madai ya fedha na migogoro ya kimapenzi, ambayo mara nyingine husababisha msongo wa mawazo kwa wanafunzi vyuoni.

Wataalamu wa saikolojia wanataja msongo wa mawazo, ukosefu wa msaada wa kisaikolojia, matatizo ya kifamilia, uhusiano wa kimapenzi na presha ya masomo,  kuwa miongoni mwa sababu kuu zinazosukuma wanafunzi kufikia hatua hizo.

Mshauri na mshunuzi, Goon Masenga, anasema ukimya wa kiakili umekithiri miongoni mwa wanafunzi wengi nchini, hali inayowaweka katika hatari ya kukumbwa na matatizo ya afya ya akili  huku wakikosa msaada.

“Kuna ukimya mkubwa wa kiakili miongoni mwa wanafunzi. Wengi wanahisi hawasikiki, hawana msaad, na hawajui wa kuongea naye,” anasema.

Anasema hata wale wanaoonekana kuwa na kundi kubwa la marafiki, mara nyingi hukosa msaada wa kweli wanapokumbwa na changamoto, jambo linaloonyesha kuwa  mtu kuwa na marafiki wengi  si kigezo cha faraja ya kiakili.

Kwa upande wake, mwalimu wa saikolojia na malezi, Modester Kimonga anasema chanzo kikubwa cha ongezeko la matukio ya kujiua kwa wanafunzi wa vyuo kikuu , kinatokana na aina ya malezi wanayopata watoto wa kizazi cha sasa.

“Mara nyingi malezi bora ni yale kutoka moja kwa moja kwa mzazi, sasa mzazi anatingwa na kazi au shughuli nyingine, hivyo humpeleka tu mtoto shule ya bweni akiwa bado mdogo. Kwa hiyo, anakosa msingi wa maelekezo ya kimaisha na namna ya kuhimili changamoto mbalimbali za kijamii na kisaikolojia,” anasema.

Anasisitiza kuwa ili kupunguza vifo hivyo, ni muhimu wazazi kuhakikisha wanatoa malezi ya karibu na bora kwa watoto wao tangu awali, sambamba na kuwajengea uwezo wa kujielewa na kukabiliana na mazingira yanayowazunguka.

Halima Msando, ofisa wa mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), anasema kizazi cha sasa kimelelewa katika mazingira tofauti na yale ya zamani, jambo linalochangia kuzorota kwa uwezo wa kudhibiti hisia na kushughulikia matatizo kwa utulivu.

“Kizazi kilichopita kilikuwa kimetulia, kimelelewa kwa maadili ya kujizuia na kuwa wavumilivu. Lakini kizazi cha leo kinaishi katika ulimwengu wa haraka unaochochewa na mitandao ya kijamii na teknolojia hali inayopunguza uvumilivu,” anasema.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Gertrude Abel, anaeleza kuwa sababu za kiuchumi na kijamii, ni miongoni mwa vichochezi vikubwa vya msongo wa mawazo kwa vijana.

“Vijana wengi wanategemewa na familia, lakini uchumi wao ni dhaifu. Wanaposhindwa kutimiza matarajio ya kifamilia na kimaisha, wanaingia kwenye msongo mkubwa wa mawazo. Hii inazidi kuongezeka hasa kutokana na mfumo wa malezi wa sasa unaotofautiana sana na wa zamani,” anasema.

Sophia Mrope, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), anasema kwa mtazamo wake, sababu kubwa inayowasukuma wanafunzi wengi kujihusisha na migogoro au hata kujiua ni msongo wa mawazo.

“Kuna pia changamoto ya upweke na ukosefu wa usaidizi wa kisaikolojia chuoni. Mwanafunzi anapopitia kipindi kigumu hana mahali pa kutolea hisia zake, na mwishowe anafanya uamuzi mbaya,” anasema na kuongeza:

“Mara nyingi jamii inaamini kuwa ukiwa chuo basi maisha ni rahisi. Lakini ukweli ni tofauti. Kuna presha ya matokeo, maisha ya kijamii, na hata uhusiano wa kimapenzi. Yote haya yakikukaba kwa wakati mmoja, yanaweza kuwa mzigo mkubwa mno kwa akili ya kijana.”

Kwa upande wake, Daniel Komba, mwanafunzi wa mwaka pili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM) anasema : “Kizazi chetu kimefungwa sana na mitazamo ya nje kupitia mitandao ya kijamii. Wanafunzi wengi wanajilinganisha na maisha ya watu wengine, jambo linalowatia presha na kuwakatisha tamaa pale wanapojiona hawafikii viwango hivyo.”

Mwanafunzi mwingine, Osibati Gidioni wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) anasema hali ngumu ya maisha chuoni,  imekuwa chanzo kikuu cha baadhi ya wanafunzi kuchukua uamuzi mgumu wa kujiua.

“Ukiingia chuoni, kila mtu anakuwa kivyake. Kuna wanaopata hela nyingi kutoka kwa wazazi au walezi wao, sisi wengine tunahangaika hadi mlo mmoja kwa siku unakuwa wa bahati. Unajikuta unajilinganisha bila kujua na mwisho wake unakosa tumaini kabisa,” anasema.

Anaongeza: ‘’Ukosefu wa msaada wa kisaikolojia kwa wanafunzi wengi, hasa  wanapopitia changamoto binafsi kama kushindwa mitihani, migogoro ya kiuhusiano, au kukosa mkopo, huongeza presha ya maisha. Wanabeba mengi kichwani, hakuna wa kuongea naye. Mwingine anacheka darasani, lakini ndani anatokwa na machozi, mwisho wake anajinyonga.’’

Matukio ya wanafunzi kujitoa uhai hayapo Tanzania pekee, ni changamoto ya kimataifa, hasa katika mataifa yanayokumbwa na presha kubwa ya kitaaluma. Kwa mfano, nchini India, zaidi ya wanafunzi 13,000 waliripotiwa kujiua mwaka 2021 pekee, 

Nchini Uingereza, ripoti za mwaka 2023–2024 zilionyesha matukio 79 vya vifo vya wanafunzi wa elimu ya juu vilivyosababishwa na kujiua.

 Kwa upande wa Korea Kusini, taifa linalojulikana kwa ushindani mkali wa kielimu, utafiti mwingi unaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya wanafunzi wa shule na vyuo,  wanakabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo, hali inayochangia matukio ya kujiua kuwa juu.

Mashirika ya haki za binadamu na ustawi wa jamii yameitaka Serikali kuanzisha kampeni maalum ya kitaifa ya afya ya akili vyuoni pamoja na kurasimisha huduma za ushauri nasaha.

Wakati vyuo vikuu vikitarajiwa kuwa ngome za maarifa, ubunifu na matumaini, sasa vimegeuka kuwa maeneo ya vilio na huzuni.

Ni wakati wa Taifa kuchukua hatua si kwa kutoa pole pekee, bali kwa kufanya kazi ya kweli ya kuokoa nafsi na ndoto za vijana wake.