125 wakamatwa wizi, dawa za kulevya Shinyanga

Shinyanga. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema kuwa jumla ya watu 125 wamekamatwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kwa tuhuma za makosa mbalimbali, yakiwemo wizi na ushiriki katika vitendo vinavyohusiana na dawa za kulevya.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari mkoani Shinyanga.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 23, 2025, katika ofisi ya Polisi ya mkoa iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Kamanda Janeth amesema kuwa watu hao wamekamatwa katika operesheni zinazoendeshwa na jeshi hilo, kwa lengo la kuwalinda wananchi dhidi ya vitendo vya uhalifu na kuhakikisha usalama wa jamii unadumishwa.

“Katika operesheni hizo vielelezo vya dawa za kulevya zilizokamatwa ni pamoja na gramu 2,261 za bangi, kilo 29 za mirungi, pombe ya moshi lita 142, bajaji moja, luninga saba, mabati 16, nondo vipande 17, vitanda vinne, redio nane na pikipiki 22 za wizi ambazo hazina namba za usajili,” amesema Magomi.

Katika kueleza mafanikio ya operesheni hizo, Kamanda Janeth amesema jumla ya kesi 25 zimefikishwa mahakamani na kutolewa hukumu.

Amesema kati ya hizo, kesi mbili za ulawiti ziliwahusisha wahalifu waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Kamanda Janeth amesema kesi mbili za ubakaji zilimalizika na wahusika kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 kila mmoja.

Pia, amesema kesi tano za uvunjaji wa nyumba na wizi zimemalizika kwa hukumu za vifungo vinavyotofautiana kati ya miezi miwili hadi miaka minne jela.

Akieleza kuhusu mwenendo wa mashauri ya jinai yaliyoshughulikiwa na Jeshi la Polisi mkoani humo, amesema: “Kesi nane za wizi zimefikishwa mahakamani, ambapo jumla ya washtakiwa 21 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo vinavyotofautiana kati ya miezi miwili hadi miaka mitatu jela.

“Kwa upande wa kesi mbili za kujeruhi, washtakiwa wote walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.

“Katika kesi nne za shambulio la kudhuru mwili, wahusika walihukumiwa vifungo vya miezi miwili hadi sita jela, huku kesi mbili za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu zikiwapa washtakiwa wanne adhabu ya kifungo cha miezi mitatu hadi sita jela,” amesema.

Kuhusu masuala ya usalama barabarani, amebainisha kuwa hatua za kinidhamu zimechukuliwa dhidi ya madereva waliokiuka sheria za usalama barabarani.

“Madereva watatu wamefungiwa leseni kwa muda wa miezi mitatu baada ya kubainika waliendesha magari kwa mwendokasi wa zaidi ya kilomita 80 kwa saa, kinyume na sheria. Madereva hao walikamatwa wakitembea kwa kasi ya kilomita 100, 101 na 118 kwa saa,” ameeleza.