HATIMAYE kipa Ali Ahamada ambaye alikuwa akiichezea KMC kwa mkopo akitokea Azam FC amefunga ukurasa wake wa kucheza soka la kulipwa nchini baada ya kumaliza mkataba wa miaka mitatu.
Ahamada ambaye alikuwa akitajwa kati ya wachezaji ghali zaidi nchini, ameondoka nchini akiacha kumbukumbu mbalimbali, lakini kubwa zaidi kwake ni mechi dhidi ya Yanga iliyochezwa Desemba 25, 2022 kwa Mkapa na Azam ilipoteza kwa mabao 3-2.
Ahamada ameweka wazi kuwa mechi hiyo iliyopigwa Krismasi ndio itaendelea kubaki kwenye akili na moyo wake kwa muda mrefu.
“Ilikuwa mechi yenye presha na kwa bahati mbaya kwangu niliruhusu mabao matatu, na yalitufanya kupoteza, niliumia kwa sababu nilihitaji kuwa msaada kwa timu yangu,” alisema.
Katika mechi hiyo, Azam ilitangulia kupata bao kupitia Abdul Hamis Suleiman ‘Sopu’ dakika ya 27, kabla Yanga kusawazisha kwa mabao ya haraka ya Fiston Mayele dakika ya 31 na Stephane Aziz Ki dakika ya 33.
Sopu alisawazisha tena kwa Azam dakika ya 47, lakini Farid Mussa alihakikisha Yanga inaondoka na pointi tatu kwa bao la ushindi dakika ya 78.
Kabla ya kujiunga na Azam, Ahamada alitokea Ulaya, akiwahi kuichezea Toulouse kwenye Ligue 1 nchini Ufaransa. Ujio wake Azam mwaka 2022 ulionekana kuwa sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kuongeza uzoefu kwenye eneo la ulinzi lakini majeraha yalimuandama kiasi cha kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kabla ya kutolewa kwa mkopo.
Kupitia ujumbe wake wa kuaga, Ahamada alimshukuru Rais wa Azam, Yusuf Bakhresa, kwa kumfungulia milango ya kucheza Tanzania. Pia hakusita kuitaja KMC kama sehemu muhimu ya safari yake ya soka hapa nchini. “Imekuwa safari yenye hisia nyingi nikiwa na Azam na KMC. Asanteni kwa kila kitu na nawatakia kila la heri!” aliandika.