Aliyeachiwa huru kwa ulawiti afungwa maisha

Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, kupitia Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imeitengua hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ambayo awali ilimuachia huru Julius Meela aliyekuwa anakabiliwa na shtaka la ulawiti.

Katika rufaa hiyo ya jinai  ya mwaka 2024 iliyokatwa na Jamhuri dhidi ya Meela, hukumu iliyotolewa Julai 18, 2025 na Jaji David Ngunyale na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama, imemkuta Meela na hatia na imemuhukumu kifungo cha maisha gerezani.

Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za rufaa na kueleza kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulithibitisha pasipo shaka kuwa Julius alitenda kosa hilo.

Meela alikuwa anashtakiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita, lakini Mahakama ya Wilaya ilimuachia huru kwa maelezo kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi hiyo bila shaka.

Hata hivyo, baada ya rufaa iliyokatwa na Jamhuri, Mahakama Kuu imejiridhisha kuwa ushahidi uliowasilishwa ulikuwa na uzito wa kumtia hatiani mshtakiwa.

Kutokana na hilo, hukumu ya awali imefutwa rasmi na adhabu ya kifungo cha maisha jela imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu.

Meela alishtakiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita, Januari 29, 2023 katika eneo la Sinza, jijini Dar es Salaam.

Awali alidaiwa kumshawishi mtoto huyo kwa kumpa simu acheze mchezo wa ‘game’.

Mahakama ya chini ilimuachia huru kwa maoni kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka.

Hata hivyo, Jamhuri ilikata rufaa kupitia Wakili wa Serikali, Debora Musi, wakidai kuwa hakimu alikosea kisheria kwa kupuuza ushahidi wa kimazingira na kwa Julius kushindwa kuwahoji mashahidi wa upande wa mashtaka.

Mahakama ilibainisha kuwa mtoto alimtaja Meela kuwa alimlawiti na alimzuia kupiga kelele kwa kumtishia kutompa tena simu.

Aidha, ushahidi wa daktari (shahidi wa nne) ulithibitisha kuwa sehemu ya haja kubwa ya mtoto huyo ilionyesha kupenyezwa kitu butu.

Mahakama ilizingatia kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu kinachotoa adhabu ya kifungo cha maisha kwa kosa la ulawiti kwa mtoto chini ya miaka 10.

Jaji Ngunyale alisema: “Kosa lilithibitishwa bila shaka yoyote. Mahakama ya chini ilifanya makosa kumuachia huru. Rufaa inakubaliwa na agizo la kuachiliwa linabatilishwa. Meela ametiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani.”

Katika utetezi wake, Julius Meela alikana kutenda kosa hilo na kudai kuwa siku ya tukio alikuwa nyumbani akitazama televisheni na jamaa zake.

Shahidi wa kwanza wa utetezi, ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa, alidai mtoto alikanusha kubakwa alipomuhoji.

Hata hivyo, Mahakama ya Wilaya ilimuachia huru Meela kwa hoja kuwa tukio halikuripotiwa siku hiyo na hakutajwa moja kwa moja na mlalamikaji, hivyo ikahitimisha kuwa kesi haikuthibitishwa pasipo shaka.

Jamhuri ilidai hakimu alikosea kwa kupuuza ushahidi wa kimazingira na kutozingatia kuwa Meela hakuwahoji mashahidi wa mashtaka kuhusu madai muhimu, hali inayomaanisha aliyakubali.

Jaji Ngunyale, akitoa uamuzi Mahakama Kuu, alisema ushahidi unaonyesha kuwa tukio lilitokea mbele ya mjibu rufaa, ambaye mwenyewe alikiri kuwepo eneo hilo.

Baada ya kupima hoja za pande zote, Mahakama ilimkuta na hatia Julius Meela na kumuhukumu kifungo cha maisha kwa kosa la ulawiti wa mtoto chini ya miaka 10, kwa mujibu wa sheria.