Dodoma. Mwili wa Frank Sanga (34) aliyefariki dunia kwa kupigwa na risasi umezikwa leo huku wachungaji wa Kanisa la Anglikana wakitaka Serikali isimamie mambo hayo yasijirudie kwa sababu yanaiumiza jamii.
Mbali na vilio vilivyotanda nyumbani hadi kanisani, baadhi ya ndugu walipoteza fahamu baada ya kuona mwili wa ndugu yao.
Mjane wa Frank Sanga aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi (wa kwanza kulia) akiwa na baadhi ya waombolezaji nyumbani kwake Matumbulu jijini Dodoma. Picha na Elidaima Mangela.
Frank alifariki dunia Julai 19,2025 baada ya kupigwa risasi katika eneo la makutano ya barabara ya mzunguko Ntyuka jijini Dodoma wakati alipokuwa katika mvutano kati ya dereva bodaboda na polisi.
Chanzo cha mvutano huo kinadaiwa kutokea baada ya dereva bodaboda, Mathias Choma (32) kukamatwa kwa kutovaa kofia ngumu, kutokuwa na leseni na kuendelesha pikipiki mbovu, ambapo aliita ndugu zake kabla ya kupelekwa kituo cha polisi. Miongoni mwa ndugu waliokuja ni Frank, ambapo kulizuka mvutano kati yao na polisi wakishinikiza ndugu yao aachiwe, polisi walifyatua risasi na mojawapo ilimpata Frank.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Frank Sanga aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi, wakiutoa mwili wake nyumbani kwake Makumbulu jijini Dodoma. Picha na Elidaima Mangela.
Akihubiri katika ibada ya mazishi katika Kanisa la Anglikana Parishi ya Matumbulu, leo Julai 23,2025, Mchungaji wa kanisa hilo, Bahi Nason Mjimbu amesema wanataka kuona kila raia anabaki salama na pindi atakapoona vyombo vya ulinzi na usalama basi akimbilie hapo.
“Hatutaki kuona yale yanayotokea katika televisheni kwenye mataifa mbalimbali…Sisi wachungaji tunapokwenda kusema katika tukio kama hili tunapata shida. Tunataka nchi hii iwe ya amani.
“Mwaka huu kwetu ni mkubwa wa uchaguzi tunaitaka Tanzania idumu katika amani, wakati wa uchaguzi na baada, jambo hili lililotukusanya litufundishe kuitafuta amani. Tanzania pawe mahali pa makimbilio,”amesema.
Ametaka wasemaji wa tukio hilo wawe wachache na kuiombea Tanzania wanapokwenda katika uchaguzi na wale waliopewa dhamana ya kulinda wananchi na mali zao kila mtu asimamie kwa nafasi zao.
“Mungu ataiongoza nchi hii katika amani sio mafarakano,” amesema.

Baadhi ya waombolezaji wakiomboleza msiba wa Frank Sanga nyumbani kwake Makumbulu jijini Dodoma. Picha na Elidaima Mangela.
Mchungaji wa Parishi ya Matumbulu ya Kanisa la Anglikana jijini Dodoma, Samson Kwanga amesema baadhi ya watu wanaweza kuwa na hofu na Serikali kwa matukio machache kama hayo.
“Kwa sababu jamii imeumia na hii isipotengenezwa jambo hili likae vizuri, jamii inaweza kutokuwa na imani na Serikali matukio machache kama haya ambayo yanaumiza kutokana na watu wachache wanaogonganisha matukio kama haya.
“Ifike mahali basi watu hawa wachache Serikali ihakikishe kuwa inasimamia mambo haya katika hali halisi bila kuwa na hofu.
Akisoma historia fupi kanisani, shemeji wa marehemu, Nathael Joshua amesema kuwa Sanga aliamka salama siku ya Julai 19, 2025 na kwenda kuchukua ng’ombe wawili kwa ajili ya kukokota mkokoteni wa maji kwenye eneo la Ntyuka Dodoma.
Amesema akiwa maeneo ya barabara ya mzunguko ya Matumbulu alikutana na askari wananyang’anyana funguo na dereva bodaboda aliyekuwa amebeba mkaa.
Amesema yule dereva bodaboda alisema ameshapata kibali cha kubeba mkaa huo katika eneo la Kibaoni.

Amesema katika tukio hilo, Sanga alipigwa risasi mguuni na familia ilipofika na kumpeleka Hospitali ya DCMC ambapo madaktari walisema ameshapoteza maisha kwa kuvuja damu nyingi.
Mmoja wa majirani, Eva Mazengo ametaka Serikali kuliangalia jambo hilo kwa makini sana na wawasaidie watoto wa marehemu wasome ili waje waikomboe familia.
Naye Mwenyekiti Msaidizi wa Mtaa wa Kusela, Festo Lumorwa amesema wameamua kuzika leo kwa baada ya kupata majibu yaliyo sahihi kuhusiana na msiba huo.
“Ili kwa vijana tunatoa funzo tusiwe na mihemko linapotokea jambo inabidi tukae pembeni kuacha Serikali ifanye kazi kwa sababu tupo viongozi watupe taarifa sisi tutafanya ushirikiano na wao, haya mambo yasiwe yanatokea mara kwa mara,” amesema.
Julai 21,2025 akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera alisema tukio la Frank kupigwa risasi lilitokea Julai 19,2025, saa 8.00 mchana Ntyuka Dodoma mjini.
“Hapa askari wetu wawili wa doria ya pikipiki walikuwa wakiendelea na doria katika maeneo hayo. Lakini, muda huo walimkamata mwananchi mmoja akiwa anaendesha pikipiki bila leseni, helmet na pia akiwa amebeba mkaa unaodhaniwa kwamba ni gunia tatu,”alisema.

Alisema mwananchi huyu alipewa maelekezo kwamba waongozane kwenda kituo cha Polisi ili makosa hayo yaweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
“Lakini alikataa kwenda kituoni akisema kwamba ni mpaka ndugu zake waje hivyo alipata fursa ya kuwapigia ndugu zake simu. Nao walikuja wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki ambazo inadaiwa ni zaidi ya tatu lakini kila pikipiki ilikuwa na zaidi ya abiria wawili,”alisema.
Alisema walipofika katika eneo la tukio walilazimisha ndugu yao aachiwe.
“Katika mazingira hayo sasa baadhi ya hao wana ndugu ambao walikuja eneo la tukio wakiwa na fimbo walianza kumshambulia askari mmoja wakimlazimisha kuutoa ufunguo au switch ya hiyo pikipiki,”alisema.
Alisema hivyo ililazimu mmoja wa askari kufyatua risasi hewani lakini baadhi waliendelea kumshambulia kwa fimbo na kuanguka chini, ilifyatuliwa risasi iliyompata Frank.
Hata hivyo, alisema askari hao wanashikiliwa huku uchunguzi unaendelea kwa kukusanya ushahidi wote unaoelezea mazingira ya tukio jinsi lilivyotokea.
Marehemu ambaye alikuwa mjasiriamali, ameacha mke na watoto wanne.