Ivory Coast. Muuguzi mmoja aitwaye Tokpa Japhet mwenye umri wa miaka 43 ametupwa jela kwa kile kilichoelezwa andiko lake la Facebook aliloandika; ‘Bara la Afrika lingenusurika endapo Rais Alassane Outtara hangezaliwa”.
Kutokana na kauli hiyo Japhet kutoka nchini Ivory Coast ametupwa jela miaka mitatu wakati ikiwa imesalia miezi miwili kabla ya taifa hilo kuingia kwenye uchaguzi mkuu mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Serikali, Oumar Kone katika taarifa yake iliyotolewa Jumatatu Julai 21,2025, amesema Japhet amehukumiwa kifungo hicho na kupigwa faini ya dola 8,500 licha ya kuomba msamaha.
Imeelezwa muuguzi huyo alienda mbali zaidi na kuandika “Mama yake Ouattara angetoa mimba angeokoa Afrika”.
Kwa mujibu wa DW, viongozi sita kutoka chama kikuu cha upinzani cha Democratic Party of Ivory Coast, (PDCI) wamekamatwa tangu Juni, kutokana na ujumbe waliochapisha mitandaoni ikitoa wito wa kuipinga serikali.
Hata hivyo, upinzani wa nchi hiyo unaishutumu serikali ya Ouattara kwa kujaribu kuzima upinzani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
Tovuti ya TRT na Arab News zimeeleza Ofisi ya mwendesha mashtaka imesema mashtaka hayo ni sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na utovu wa nidhamu kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linaongezeka mara kwa mara.
Pia, imeelezwa mtu mwingine aliyejulikana kama Moussa Diakate, alikamatwa baada ya kuchapisha video ya vitisho vya kifo dhidi ya wafuasi wa kisiasa.
Katika hatua nyingine Rais Ouattara (83), hajathibitisha iwapo atawania muhula wa nne, ingawa amependekezwa na chama chake kufanya hivyo.
Ivory Coast, taifa la Afrika Magharibi ambalo lilianza kukumbwa na ghasia mara kwa mara wakati wa uchaguzi baada ya mapinduzi ya kwanza ya nchi hiyo mwaka 1999.
Aidha, mwishoni mwa 2010 na mwanzoni mwa 2011, ghasia zinazohusiana na kura ya maoni zilisababisha vifo vya watu 3,000 baada ya rais wa wakati huo Laurent Gbagbo kukataa kutambua ushindi wa Ouattara katika uchaguzi.