Baridi ilivyoleta athari kiafya, kiuchumi wizara yatoa tahadhari

Dar es Salaam. Ongezeko la baridi katika msimu huu wa kipupwe katika baadhi ya maeneo nchini Tanzania, umeleta athari za kiafya na kiuchumi huku, Wizara ya Afya ikitoa tahadhari dhidi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

Magonjwa hayo ni pamoja na maambukizi ya njia ya juu ya hewa kwa watoto, kikohozi, mafua (Influenza) pumu, nimonia inayoathiri zaidi wazee na watoto na kuvimba kwa njia za hewa ‘Bronkitisi’, kupata mzio na kukauka kwa ngozi/kupasuka.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi msaidizi wa epidemiolojia na udhibiti wa magonjwa kutoka Wizara ya Afya, Dk Vida Mmbaga amesema katika msimu huu ni muhimu kujikinga na baridi na kukinga kundi la watoto na wazee dhidi ya nimonia.

Amesema msimu huu kumekuwa na ongezeko la mafua yanayosababishwa na virusi vya influenza.

Dk Vida amesema wale ambao kwa kawaida kinga ya mwili inashuka wakiwemo watoto, wazee na wenye magonjwa nyemelezi ambao kinga iko chini wanaweza kupata mafua hayo kwa ukali zaidi.

“Kuna wakati Influenza huongezeka kama msimu huu wa kipupwe hivyo jamii inashauriwa wakati huu wa baridi, kuyakinga makundi ya watoto na wazee kwa njia mbalimbali, ikiwamo kuvaa nguo za kuwakinga na baridi, kwani virusi hivi wakati wa baridi ndipo hustawi,” amesema.

Amesema katika msimu wa baridi, kuna magonjwa mengi huibuka ikiwemo nimonia, pumu na magonjwa ya mfumo wa upumuaji kwa ujumla.

Ameshauri wananchi wanapaswa kufika katika vituo vya afya ili kupimwa na kupata matibabu sahihi wanapopata mafua, kwani wakati mwingine inasababisha hata nimonia, kutoka na baridi lililoongezeka.

Baadhi ya waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda mkoani Njombe akiwemo Onesmo Ng’ang’ane amesema uwepo wa baridi kali umekuwa ukiwaathiri kiafya na hata kibiashara.

“Wateja wapo lakini mara nyingi wanaacha kupanda bodaboda wanakwenda kwenye bajaji kwakuwa imefunikwa kwa hiyo baridi haiwakuti sana sasa hii inatuathiri kukosa wateja,” amesema Ng’ang’ane.

Mwendesha pikipiki maarufu katikati ya Jiji la Dodoma, Juma Ali (Mpemba) amesema wameathirika pakubwa kwani wateja wao nyakati za usiku wanawakimbia.

Mpemba amesema ikifika saa mbili usiku, watu hawatumii pikipiki wanakimbilia kwenye bajaji.

“Utakuta mtu anapenda kutumia usafiri wa bodaboda, lakini hili baridi anaamua kuahirisha na kupanda bajaji, pia wafanyabiashara wa makoti wanatuumiza sana, makoti yaliyouzwa Sh8,000 sasa wanatuuzia Sh15,000,” amesema Mpemba.

Kwa upande wao baadhi ya bodaboda mkoani Arusha, wameeleza msimu huu wa baridi wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu.

Mmoja wa madereva hao, Joachim Isaya amesema kipindi hiki hasa nyakati za asubuhi na usiku wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na hali ya hewa.

“Kiukweli kama unavyoona hapa nimelazimika kuweka hii karatasi laini mbele, ili inisaidie kupunguza baridi hasa nyakati za asubuhi na usiku, baridi imekuwa kali tunafanya kazi kwenye mazingira hatarishi ila hakuna namna,” amesema.

Naye Ramson Kimario, amesema amelazimika kupunguza muda wa kufanya kazi kutokana na hali ya hewa, ambapo awali alikua akianza kazi saa 11 alfajiri hadi saa sita usiku ila kwa sasa amepunguza muda huo.

“Kiukweli nimeanza kushuka kiuchumi kwani imebidi nipunguze muda wa kuanza kazi kutoka saa 11 alfajiri hadi saa moja na usiku nafanya mwisho saa mbili, kwani mazingira ya huku nje ya mji ninakopeleka wateja ni ya baridi sana,” amesema.

Mmoja wa wazee wa eneo la Moshono, Anne Christopher amesema kipindi cha msimu wa baridi kali kama ilivyo sasa mkoani Arusha imekuwa ikimsumbua na kumsababishia madhara kiafya.

Amesema amelazimika muda mwingi kujifungia ndani akijikunyata kwenye moto kama njia ya kupambana na baridi hiyo.

“Ninaogopa na umri huu kupata matatizo kama ya upumuaji na magonjwa ya viungo nalazimika kutumia muda mwingi kukaa ndani, pale inapobidi ili nisije kupata madhara yatokanayo na baridi kali hasa msimu huu,” amesema.

Muuza Makoti katika soko la Sabasaba Dodoma, Anthony Chami amesema kipindi hiki kwao ni neema na ndiyo msimu wa kupata faida kubwa.

Chami amesema hakuna biashara nzuri kwa sasa sokoni hapo zaidi ya makoti na majaketi licha ya kukiri kuwa ni biashara ya msimu na ukifika wakati, huwa haitoki kabisa na amekiri bei ya bidhaa hiyo ipo juu zaidi ya mara mbili kwa bei za kawaida.

Naye mkazi wa Njombe, Dora Deule amesema kwa sasa hivi kuna baridi kali tofauti na miaka mingine hali inayowafanya kuvaa nguo nyingi ili kujikinga na baridi.

“Kuna wengine wanatumia vifaa vya umeme ili kupata joto lakini wengine wanakoleza mikaa japo wanachukua tahadhari zaidi, wanaota lakini muda wa kulala ukifika wanatoa moto nje na kufungua madirisha ili hewa itoke kisha wanaingia kulala,” amesema Deule.

Wananchi wa Mafinga mkoani Iringa wamelalamikia hali ya baridi kali inayoendelea kuikumba sehemu hiyo, wakisema imeathiri afya na shughuli zao za kila siku.

‎Wengi wao wakizungumza na Mwananchi jana Jumanne, Julai 22, 2025 wameeleza nyakati za asubuhi hali huwa mbaya zaidi ambapo hulazimika hata kuota moto kabla ya watoto kwenda shule au wao kwenda kazini.

‎Kwa upande wa kiuchumi, wafanyabiashara wa mbao kutoka Ifwagi Mafinga mkoani Iringa, wamesema kuwa baridi kali iliyoambatana na ukungu inasababisha mbao kulowana, hali inayowafanya wafanyakazi kushindwa kuzibeba au kuzisafirisha kwa wakati.

‎”Ukungu mzito husababisha ucheleweshwaji wa mizigo, jambo hili huathiri uzalishaji na usafirishaji wa mbao kutoka viwandani kwenda sokoni, hali hii imesababisha hasara kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitegemea mapato ya kila siku,” amesema Gwamaka Kalinga

‎Naye Khadija Mbata, mmoja wa wajasiriamali wa bidhaa tofautitofauti mjini Mafinga, amesema kuwa baridi kali iliyokuwepo wiki moja iliyopita ilifikia kiwango cha kutisha ambapo hata kufungua duka saa 12 asubuhi ilikuwa changamoto.

‎”Kwa kweli baridi ipo hasa wiki ile iliyopita nilikuwa nashindwa hata kukunjua mikono kwa sababu ya baridi kali, jambo lililonilazimu kuchelewa kuanza kazi na kupoteza wateja wa asubuhi, ” amesema Khadija.

Hata hivyo wananchi wameshauriwa kutumia njia sahihi za kukabiliana na baridi ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kujitokeza ikiwemo watu kupoteza maisha.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya mji wa Njombe, Dk Jagadi Ntugwa amesema njia nzuri za kujilinda na baridi ni pamoja na kuvaa nguo nzito, huku wakihakikisha wanakuwa katika chumba chenye hewa ya kutosha.

Amesema wapo ambao wanatumia vifaa vya umeme kama njia salama ya kujikinga na baridi, kwa kuwa vifaa hivyo vinatoa joto na ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Amesema zipo njia siyo sahihi watu huzitumia katika kujikinga na baridi mfano matumizi ya jiko la mkaa ambapo mkoani Njombe, imekuwa kawaida kwa watu kutumia njia hiyo kujikinga na baridi.

“Tumeshasikia matukio mengi huku Njombe unakuta mtu anajifungia na jiko la mkaa sasa jiko la mkaa linatoa gesi ya monoxide ambayo inakwenda kushindana na hewa ya oksijeni kwenye seli nyekundu za damu, ndiyo maana mtu anapata yale madhara anapoteza maisha,” amesema Ntugwa.

Amesema matumizi ya majiko katika kujikinga na baridi yanaweza kusababisha madhara mengine makubwa kama kuchoma nyumba na vitu vingine.

Amesema elimu imeendelea kutolewa kwa wananchi namna ya kujikinga na baridi kupitia vyombo vya habari na kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali.

Amesema hata ambao wamekuwa wakifika katika vituo vya afya baada kupata madhara, wamekuwa wakipewa elimu ili kuepuka madhara zaidi.

Amewataka wananchi mkoani humo kunywa maji kwa wingi, licha ya kuwepo kwa baridi kwani kutawaepusha na magonjwa mbalimbali ikiwemo figo kuwa na mawe.

Imeandikwa na Seif Jumanne (Njombe) Habel Chidawali (Dodoma) Janeth Mushi (Arusha) na Christina Thobias (Iringa)