BILA ‘PPP’ MAENDELEO YATAKAWIA – BALOZI DKT. MWAMPOGWA

………..

 NA MWANDISHI WETU, TANGA

Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (Public and Private Partnership – PPP) ni muhimu sana katika kuchagiza kasi ya maendeleo na bila ushirikiano huo, maendeleo yatakawia kuwafikia wananchi kule walipo.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wazalendo Huru Tanzania – Watoto wa Afrika, Balozi Dkt. Mohamed Bakari Mwampogwa, Julai 23, 2025 Jijini Tanga, alipokuwa akizungumzia umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta hizi mbili kwani mahitaji ya wananchi ni mengi. 

Amesema serikali pekee haitamudu kumaliza changamoto za wananchi endapo sekta binafsi itabaki nyuma au kutoshiriki kabisa katika kuunga mkono programu za maendeleo ya wananchi na ustawi wao.

“Serikali ina wajibu wa msingi wa kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo, lakini ni vyema sekta binafsi ikawa mstari wa mbele kuunga mkono mikakati ya maendeleo, bila kufanya hivyo kutasababisha kukawia kwa maendeleo,” amesema Balozi Dkt. Mwampogwa.

Katika mkazo wake, Balozi Dkt. Mwampogwa amesisitiza kuwa maendeleo yakipatikana, ni furaha kwa jamii yote na kila mwananchi atakuwa sehemu ya wanufaika na maendeleo hayo, hivyo ni vizuri watu binafsi, taasisi, kampuni na mashirika kuwa sehemu ya wadau wa maendeleo na hapo ndipo kasi ya maendeleo itakuwa kubwa zaidi.

Katika hatua nyingine, Balozi Dkt. Mwampogwa ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imetengeneza mazingira rafiki kwa sekta binafsi kufanya shughuli zao, jambo linalosaidia sekta binafsi kuunga mkono programu mbalimbali za maendeleo hasa katika nyanja za elimu, maji, umeme, barabara, masoko, biashara na viwanda.