BODI YA TMA YAFANYA ZIARA YA KIKAZI RADA YA HALI YA HEWA BANGULO, PUGU NA KITUO CHA HALI YA HEWA JNIA

BODI ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imefanya ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa Mamlaka katika kituo cha Rada ya Hali ya Hewa, Bangulo, Pugu na Ofisi za TMA zilizopo katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam, tarehe 23 Julai 2025.Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Jaji Mshibe Ali Bakari na Makamu Mwenyekiti, Dkt. Emmanuel Mpeta.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Jaji Mshibe alisema lengo la ziara ni kukagua na kutathmini usimamzi na utendaji kazi wa miundombinu ya TMA na kutathmini utekelezaji wa Maagizo na Maelekezo ya Bodi katika kuboresha huduma na pia kutambua changamoto zilizopo, na kuona Taasisi ilipo na inapoelekea. “Bodi imekuwa ikitoa maelekezo hivyo leo ilikuwa ni siku maalum kuangalia utekelezaji wake”.Alisema Jaji Mshibe.

Alisisitiza kuwa TMA ya sasa imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya utoaji huduma. Aidha, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuiwezesha Mamlaka kwa miundombinu ya kisasa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi Dkt, Ladislaus Chang’a aliishukuru Bodi kwa kutembelea na kujionea utendaji kazi wa Mamlaka katika Uangazi, Uchakataji wa data na utoaji wa utabiri na kujionea miundombinu ya Kisasa ambayo Serikali imeiwezesha TMA kuipata. Pia alishukuru Bodi kwa maelekezo ambayo wamekuwa wakiyatoa kupitia vikao mbalimbali vya bodi, na kuiwezesha TMA kuendelea kuwa bora.

Akitoa ufafanuzi wa faida za uwekezaji wa miundombinu ya kisasa katika sekta ya hali ya hewa nchini alisema “ Kupitia rada za hali ya hewa, Mamlaka imefanikiwa kuboresha utabiri wa hali ya hewa pamoja na kuendesha mafunzo ya rada kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, wataalamu wa hali ya hewa kutoka nchi 10 za Afrika Mashariki na Kati walipata mafunzo mjini Mwanza , Tanzania na kuendelea kuipa heshima kubwa nchi yetu”.

Aliongeza kwa kufafanua kuwa, Serikali imeendelea kuhakikisha usimamizi wa mitambo hii ya kisasa inakuwa endelevu kwa kuajiri na kuwezesha wataalamu kupata mafuzo husika, ambapo mpaka sasa TMA ina wahandisi 30.

Katika hatua nyingine wajumbe wa Bodi walipata fursa ya kutembelea Kompyuta Kubwa ya Kisasa (Computer Cluster) yenye uwezo mkubwa wa kuchambua na kuchakata taarifa za hali ya hewa na kuimarisha utoaji utabiri katika maeneo madogomadogo na mahsusi kwa haraka na usahihi zaidi.