Camara bado yupo Simba | Mwanaspoti

BAADA ya tetesi na sintofahamu juu ya hatma yake msimu ujao, kipa namba moja wa kikosi cha Simba, Moussa Camara inadaiwa hivi karibuni atamalizana na mabosi wa timu hiyo kwa kusaini mkataba wa kuendelea kusalia kwenye timu hiyo.

Camara ambaye alitua Simba mwanzoni mwa msimu wa 2024-2025, amekuwa kipa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha timu hiyo kinachonolewa na Kocha Fadlu Davids huku akiwaweka benchi Ally Salim, Hussein Abel na Aishi Manula na Ayoub Lakred walioondoka.

Kabla ya Camara kuandaliwa mkataba mwingine, Simba ilishaanza harakati za kutaka kusajili kipa mwingine na kulikuwa na majina mawili mezani, Issa Fofana wa Al Hilal ya Sudan ambaye bado ana mkataba wa miaka miwili na timu hiyo na Drissa Bamba wa Stade d’Abidjan ya Ivory Coast.

Mkataba wa sasa wa Camara unatarajiwa kumalizika Julai 30 mwaka huu, lakini Simba inataka kuhakikisha inamsainisha mwingine kabla ya muda huo na tayari makubaliano yameshafikiwa na kinachosubiriwa ni yeye kuwasili nchini kutia saini.

Chanzo kutoka ndani ya Simba kililiambia Mwanaspoti: “Kocha alishaamua kumbakisha Camara, siku mbili hizi atasaini mkataba ambao kama siyo wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine basi itakuwa ni miaka miwili.

“Kila kitu kilishakuwa sawa, kuhusu mapungufu yake uwanjani makocha walisema watayafanyia kazi na wana matumaini ataendelea kuimarika.”

Licha ya kuwa na makosa kadhaa msimu uliopita, Camara alionesha kiwango bora katika mechi za kimataifa ambako Simba ilifanikiwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya RS Berkane.

Mechi ambayo alionyesha kiwango bora zaidi ilikuwa ni ile ya robo fainali dhidi ya Al Masry, ambapo aliokoa penalti mbili wakati Simba ikipata nne na kusonga nusu fainali.

Mbali na kimataifa, Camara ndiye ameibuka kinara wa clean sheet katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 alipocheza mechi 28 kwa dakika 2,520 na kuruhusu mabao 13 akiwa na clean sheet 19.