Hatari kwa wapenda intaneti ya bure

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, baadhi ya watu hupenda kutumia huduma ya mtandao wa intaneti ya bure (Free Wi-Fi) popote pale wanapoikuta, sababu ikitajwa ni kushindwa kumudu gharama za vifurushi au ni mazoea.

Hata hivyo, imetahadharishwa kuwa, kuna hatari ya matumizi ya mtandao wa aina hiyo, hasa simu kupekuliwa bila mwenyewe kufahamu.

Mwananchi imezungumza na wataalamu sambamba na kurejea maandiko ya kiusalama wa mtandao na kubaini hatari hiyo inawezekana watumiaji wa Free Wi-Fi wasiijue.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ilitoa onyo kuhusu hatari ya kutumia Wi-Fi za bure, hasa kwenye maeneo ya umma huku ikieleza matumizi hayo yanaweza kuweka taarifa binafsi za watumiaji hatarini kutokana na uwepo wa wahalifu wa mtandao.

Akinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari, Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa PDPC, Innocent Mungy alisema wahalifu wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za kidijitali kuingilia mawasiliano ya watu wanaotumia Wi-Fi za bure.

Mungy alisema hayo wakati wa mafunzo maalumu kwa maofisa ulinzi wa taarifa binafsi, alisema licha ya kuwa na mvuto kwa watumiaji, mitandao ya bure ni hatarishi kwa kuwa mara nyingi hutumiwa na wadukuzi kuiba taarifa binafsi kutoka kwenye vifaa kama simu janja na kompyuta mpakato.

Wahalifu wa mtandaoni wanaweza kutumia mbinu hiyo kuingilia mawasiliano ya watu na kunasa taarifa nyeti kama neno siri, taarifa za benki na nyaraka za kikazi.

Kiuhalisia Wi-Fi ya bure inavutia hasa katika maeneo kama vile hoteli, viwanja vya ndege, migahawa, vituo vya mabasi au maduka makubwa, ndio maana baadhi ya watu hupenda kuitumia.

Hatari ya kiusalama wa taarifa binafsi na kifaa chako unaanzia pale wadukuzi wanaweza kuiba nywila (passwords), maelezo ya benki (namba ya kadi ya ATM), taarifa za akaunti za mitandao ya kijamii au barua pepe na ujumbe binafsi.

Pia, kuna mbinu mbalimbali anazoweza kutumia mdukuzi ikiwamo kufungua mtandao bandia kwa ajili ya kuwanasa watu.

Pia, anaweza kuweka Wi-Fi yenye jina linalofanana na la eneo halisi, mfano: “Hotel_Free_WiFi” lakini si halali, lakini ukijiunga tu wanapata ufikiaji wa kifaa chako na mawasiliano yako yote.

Vilevile ipo mbinu inayojulikana kama (Man-in-the-Middle attacks) ambayo mtu wa kati anaweza kuona na kurekodi kila kitu unachotuma au kupokea mtandaoni hata kama unaona upo salama.

Pia, baadhi ya mitandao ya bure haina usimbaji wa data (encryption), hivyo mtu yeyote aliye kwenye mtandao huo anaweza kufuatilia shughuli zako bila ulinzi wowote.

Pia, inawezekana kusambazwa kwa Virusi au Malicious Software pale wahusika wanaweza kueneza programu hatari kama vile spyware, ransomware au keyloggers (zinazorekodi unachokiandika) kwenye kifaa chako bila wewe kujua.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatato Julai 23, 2025 mdau wa haki za kidijitali, Francis Nyonzo amesema ukijiunga na mtandao huo unakuwa katika hatari kwa kuwa umejiweka katika nafasi ya wadukuzi kukuingilia (kuwapa access).

Amesema kwa kuwa mtandao huo uko huru mtu mwingine pia, anaweza akaseti vitu vyake kisha akaanza kuweka mitego ya kukamata ‘packets’ zinazotumwa kutoka sehemu moja hadi nyingine, hivyo akitega anaona watu wanaotumia mtandao huo wanawasiliana nini.

“Kama kuna ulazima wa kujiunga na Wi-Fi ya sehemu husika basi utumie matumizi ya mtandao binafsi (Virtual Private Network) ili zile packets zisiweze kuonekana kwa maana zinafungwa yaani zinalindwa. Ukiwa huna VPN ni rahisi kuonekana,” amesema.

Pia, amesema mtu anapokuwa mtandao ni haki yake kulinda faragha zake, hivyo katika haki za kidijitali lazima tuangalie upya matumizi ya VPN.

Wakati anayasema hayo ikumbukwe, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilipiga marufuku matumizi ya VPN kwa wasiokuwa na kibali na anayegundulika atakumbana na adhabu ya faini au kifungo jela.

Taarifa ya katazo hilo ilitolewa Oktoba 13, 2023 kwa kuzingatia Kanuni ya 16(2) ya Kanuni ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kuhusu maudhui mtandaoni ya mwaka 2020, mtu hatatoa, hatamiliki na hatasambaza teknolojia, programu tumizi au kitu chochote kinachoendana, kinachoruhusu au kumsaidia mtumiaji kupata maudhui yaliyokatazwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Koncept Group, Krantz Mwantepele amesema changamoto kubwa inakuja pale watu wasiokuwa waaminifu kudukua taarifa zao pale anapoingia kwenye akaunti yako ikiwamo e-mail, akaunti za benki akajifanya yeye ndio mmiliki.

“Ukienda kwenye Free-Wi-Fi basi fungua vitu vya kawaida na kama simu au kompyuta  yako ina taarifa zako binafsi za kifedha anaweza akaingia akipata credit kazi za mtandao unazotumia kufanya malipo, akakuibia hela.

“Usalama wa mtandao huo, unakuwa wazi unaweza ukadukuliwa akaunti yako ikatumika kwa matumizi mabaya. Sishauri sana watu kutumia Free Wi-Fi na kama anatumia ahakikishe aingie kwenye maeneo yasiyo na password zake,” ameshauri.

Akielezea namna ya kuepuka, Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), William Sunguya amesema kwanza watu wanapaswa kuepuka aina hiyo ya mtandao kwa kuwa unapotumia unawapa mwanya watu wenye nia ovu.

Aligusia mfano ukitumia Free Wi-Fi kisha ukaingia kwenye ‘link’ (kiunganishi) ambazo ziko mtandaoni unaweza ukadukuliwa.

“Unapaswa kwanza kufahamu viashiria vya hatari ikiwamo kuingia kwenye viunganishi visivyoeleweka, kwa hiyo watu wanapaswa kuepuka kubonyeza link hizo wasizokuwa na uhakika nazo,” amesema.

Alisema unapaswa kutumia VPN (ukiwa umesajiliwa) ili kulinda taarifa zako, unapaswa kuepuka kuingia kwenye benki au akaunti nyeti ukiwa kwenye Wi-Fi ya bure. Zima “auto-connect to Wi-Fi” kwenye kifaa chako.

“Unapaswa kutumia tovuti zilizo na HTTPS, weka antivirus na firewall kwenye simu au kompyuta yako. Toa Wi-Fi baada ya kumaliza kuitumia na usikae umeunganishwa bila sababu.”