Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imesema itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaofanya kazi za habari bila kukidhi vigezo vya kitaaluma na kusajiliwa rasmi, ikisisitiza lengo ni kulinda hadhi ya taaluma ya habari nchini Tanzania.
Julai 18, 2025 bodi hiyo iliwazuia kufanya kazi watangazaji wanne wa redio ya Mjini Fm ya jijini Dar es salaam kwa kufanya kazi ya utangazaji kinyume cha kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma ya Habari kinachowataka wanahabari kusajiliwa na kupata ithibati.
Mtu yeyote anayefanya kazi za kihabari kama mwandishi, mtangazaji, waandaaaji wa vipindi, wapigapicha na wachakataji wengine wa habari ili wapate ithibati wanapaswa kuwa na taaluma ya uandishi wa habari kuanzia ngazi ya Diploma.
Hata hivyo, ufuatiliaji wa Mwananchi umebaini kuna idadi kubwa ya wanahabari na watangazaji maarufu kwenye redio na televisheni ambao wamejiweka kando baada ya kupoteza sifa kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria.
Leo Jumatano, Julai 23, 2025, Mwananchi limemtafuta Kaimu Mkurugenzi wa JAB, Patrick Kipangula kujua kinachoendelea kwenye usajili huku akisema hadi sasa kuna watu 10 wameondolewa rasmi kwenye taaluma ya habari baada ya kubainika walikuwa wakifanya kazi hiyo bila kuwa na sifa au ithibati.
Kipangula amesema taarifa zaidi walizonazo ni za waandishi wa habari waliosajiliwa ambao wamefikia 3,000 huku akieleza kuwa, usajili na ufuatiliaji unaendelea kufanyika.
“Tunaendelea na ukaguzi na ufuatiliaji wa karibu kwa wanahabari walioko kazini. Kwa wale tunaowafikia na kubaini hawana sifa za kitaaluma wala usajili, tunawatoa moja kwa moja,” amesema.
Kipangula amesema baadhi ya watu wamejitoa wenyewe kwenye taaluma hiyo baada ya kubaini hawatimizi masharti yanayohitajika kisheria.
“Kuna waliokuwa wakifanya kazi bila kuwa na sifa, wengine wakiwa na elimu isiyo husiana na habari. Baada ya kuelewa miongozo ya kisheria, wameamua kujitoa wenyewe,” amesema Kipangula.
Hata hivyo, Kipangula hakutaka kuzungumzia hilo kwa kile alichoeleza hana taarifa za kutosha na hawezi kutaja majina.
“Ninyi wenyewe si mnaona, kuna wanahabari na wengine watangazaji siku hizi hawasikiki, hatuwezi kusema moja kwa moja wamejitoa kwa sababu ya kukosa ithibati maana anaweza kusema niko likizo lakini hili suala lipo, tunachoendelea kusisitiza watu wazingatie matakwa ya kisheria,” amesema Kipangula.
Mmoja wa watangazaji wa redio moja nchini ambaye hakutaka jina lake liandikwe amekiri kituo chao kimepata pigo kufuatia kuwapoteza watangazaji wake maarufu watano kwa sababu ya kukosa ithibati.
Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari (Jowuta), Suleiman Msuya amesema kinachofanywa na JAB ndicho kitawafanya wanataaluma kufanya kazi kwa usalama na uhuru na tasnia ya habari itaheshimika kama ilivyo kwa tasnia nyingine.
“Ili kuepuka kuwa na watu ambao tunasema ni wenzetu halafu hawajapitia misingi ya kazi yetu hatuwezi kufanikiwa. Ni muhimu kuzingatia suala zima la taaluma haiwezekani kila mtu mwenye uwezo wa kuandika, kuchambua na kutangaza wawe waandishi wa habari.
“Sisi kama chama cha wafanyakazi kwenye vyombo vya habari tunaunga mkono kinachofanyika ili kuheshimisha tasnia ya habari. Sheria ilishapitishwa na ikatoa muda watu wakasome lakini bado kuna ambao hawakuitumia fursa hiyo kwa hiyo wamekiuka sheria,” amesema.
Msuya amesema ifike pahala wamiliki wa vyombo vya habari kama wanahitaji kuwatumia watu waliokosa sifa wawajibike kuwasomesha na sio kuwaruhusu waendelee kutumika kwenye sekta ya habari kwa sababu ya vipaji.
Maumivu ya rungu hilo hayawagusi wanahabari pekee bali pia wamiliki wa vyombo vya habari kama ilivyoelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Samwel Nyalla.
Akizungumza na Mwananchi, Nyalla amesema upo uwezekano wa uzalishaji kwenye baadhi ya vyombo vya habari ukapungua kutokana na kupoteza wafanyakazi.
“Kama wafanyakazi wanaondoka ni dhahiri uzalishaji wa maudhui kwenye chombo husika unaweza kupungua, hili linaweza kutokea zaidi kama waandishi au watangazaji wazoefu wakaondoka, sio rahisi kupata wapya ambao wanaweza wakaingia wakiwa na uzoefu ule ule,” amesema.
Katika hilo, amesema:“Nafikiri wangepewa muda ili waweze kukidhi matakwa ya bodi wakiwa kazini, unapomuondoa mtu kazini ataathirika kwa kupoteza kipato, kama aliajiriwa Serikali itapokosa kodi hapo na hata mchango wake kitaaluma tutaukosa.”
Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Kanaeli Kaale amesema kuna uwezekano wa tasnia kupata mtikisiko kwa kuwapoteza wazoefu wengi kwa pamoja hivyo ni vyema busara ikatumika kuwanusuru.
Amesema busara hiyo ihusishe kutengenezwa kwa programu maalumu watakayosoma ili kuwawezesha kupata vyeti vinavyokidhi matakwa ya ithibati ndani ya muda mfupi.
“Ushauri wangu ufanyike mpango wa kuwa na chuo kwa ajili ya kutoa programu maalumu kwa hawa watu ndani ya muda mfupi kwa maana asikae chuoni katika ule muda wa kawaida wa program,” amesema Dk Kaale.
“Busara itumike kitafutwe chuo kimoja wapo itengenezwe programu maalumu ambayo itawawezesha kupata vyeti. Ukipoteza watu wengi wenye uzoefu ukaingiza wengi wenye elimu mambo yanaweza yasiende vizuri.
“Kuna uzoefu na elimu, hata kama una uzoefu elimu ni muhimu. Kama huna elimu ya kutosha huwezi kuwa na fikra tunduizi. Kuna muda ulitolewa wa miaka mitano ili watu wakasome lakini wakashindwa kuitumia.”