Kampeni ya Mama Samia Legal Aid imeendelea kuleta mafanikio makubwa katika kusogeza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wa kawaida nchini kote, huku wengi wao wakipata haki walizokuwa wakizikosa kutokana na ukosefu wa elimu ya sheria na uwezo wa kifedha.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, amesema kampeni hiyo imeleta mabadiliko chanya lakini bado kuna changamoto katika maeneo ya vijijini.
“Licha ya mafanikio tuliyoyapata, bado kuna maeneo mengi nchini ambako wananchi hawajui haki zao wala njia za kuzidai,” alisema.
Maswi amesisitiza kuwa ili kufanikisha lengo la haki kwa wote, kuna haja ya kushirikisha sekta binafsi, mashirika ya kiraia na viongozi wa jamii ili kufikisha elimu ya kisheria kwa wananchi walioko pembezoni.
Kwa upande wake, Hanifa Ramadhan Said, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kutoka Ofisi ya Rais, alisema kampeni hii imeimarisha uhusiano kati ya serikali na wananchi.
“Tunaona kwa sasa wananchi wanakaribia zaidi serikali kwa sababu wanajua kuna masikio yanawasikia,” alieleza.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, alisema ipo haja ya kutumia mbinu jumuishi katika kutoa msaada wa sheria.
“Tunahitaji mawakili wa kujitolea, taasisi za kijamii na serikali za mitaa kushirikiana kwa karibu kuhakikisha mtu wa mwisho kabisa kijijini anapata msaada wa kisheria,” alisema.
Baadhi ya changamoto zilizobainishwa ni pamoja na uhaba wa wanasheria vijijini, ukosefu wa vituo vya msaada wa sheria, na wananchi wengi kutofahamu kuwa huduma hizi hutolewa bure kupitia kampeni hiyo.
Kampeni ya Mama Samia Legal Aid inaendelea kuungwa mkono na taasisi mbalimbali kama ishara ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha haki inapatikana kwa wote bila kujali hali ya kiuchumi wala kijiografia.