KMC na Bittech Zatembelea Faraja Orphanage Centre – Global Publishers


Jumatano ya leo imeanza vyema kabisa kwenye kituo cha watoto yatima cha Faraja Orphanage Centre kule Mburahati Maziwa baada ya kupokea ujio wa Bittech na KMC ambao walifika kwaajili ya kutoa msaada kwa watoto hao.

Kituo hicho cha Faraja Orphanage Centre kina watoto wengi ambao pia wanahitaji msaada kutoka sehemu mbalimbali kwani hata kwenye vitabu vya dini imeandikwa kuwa tuwajali watoto yatima na wale ambao wapo kwenye mazingira magumu.

Hivyo kwa kuona hilo kampuni ya kiteknolojia ya Bittech ambayo ipo jijini Dar es salaam kwa kushirikiana na klabu ya mpira wa miguu KMC ya Kinondoni wlaiona kwa pamoja wafike kituoni hapo na kutoa msaada wa vifaa vya shule kama vile madaftari, mabegi ya shule, kalamu, penseli, na vifaa vingine vya msingi vya kujifunzia, yote hayo ni kwaajili ya kuwafanya watoto waendelee na masomo yao kwa ari na morali mpya.

Elimu ni ufunguo wa maisha hivyo kila mtoto anapaswa kuipata elimu hiyo kwa hali na mali ili iweze kumsaidia  hapo baadae. Vifaa hivyo ambavyo Bittech na KMC wamewapatia watoto kwenye kituo hicho cha Faraja Orphanage Centre vitawasaidia kwenye msomo yao.

Kwa upande mwingine, mchezaji mwakilishi kutoka klabu ya KMC FC alieleza kuwa timu hiyo inathamini nafasi yake katika jamii na ina jukumu la kuwa mfano wa kuigwa ndani na nje ya uwanja akisema kuwa, “Soka ni zaidi ya mchezo. Ni sauti ya matumaini. Kama timu ya wananchi, tumeamua kuwa karibu na jamii na kugusa maisha ya wale wanaotufuatilia na kutuunga mkono.”

Walezi wa kituo cha Faraja Orphanage Centre walionesha furaha na shukrani kubwa kwa msaada huo na kwa uwepo wa wawakilishi kutoka Bittech na KMC FC, wakisema kuwa msaada huo umewatia moyo na kuwapa sababu mpya ya kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kulea watoto kwa upendo na kujitolea, “Tunapokea msaada huu kwa mikono miwili. Asanteni kwa kutuona, kutusikiliza na kutukumbuka,” alisema mmoja wa walezi wa kituo hicho.

Kupitia ushirikiano kama huu, Bittech na KMC FC wanaonyesha kuwa maendeleo ya jamii hayawezi kufanikishwa na serikali pekee, bali kwa nguvu ya pamoja kati ya sekta binafsi, michezo, na wadau wa maendeleo.