Kocha Mfaransa atua Yanga na jembe jipya

KLABU ya Yanga imeendelea kuboresha benchi lake la ufundi kwa kufanya usajili mwingine muhimu, safari hii ikimleta kocha mkongwe wa makipa kutoka Tunisia, ambaye anatarajiwa kuungana rasmi na Kocha Mkuu, Romain Folz raia wa Ufaransa.

Kocha huyo wa makipa anayekuja kuchukua nafasi ya Alae Meskini aliyetimkia AS FAR Rabat ya Morocco tangu Februari 19, 2025, anaitwa Majdi Mnasria ambaye mwaka jana aliondoka Lamontville Golden Arrows ya Afrika Kusini. Kocha huyo ana uzoefu mkubwa ambapo aliwahi kuwa na vipindi viwili vya kazi katika klabu hiyo ya Durban.

Kuwasili kwake katika klabu ya Yanga kutakuwa na umuhimu mkubwa, hasa wakati huu ambapo timu hiyo inajipanga kuuanza msimu wa 2025-2026 kwenda kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ililolitwaa kwa misimu minne mfululizo. Vilevile, atakuwa sehemu ya kusaka mafanikio kimataifa Yanga itakaposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Mnasria ni kocha mwenye uzoefu mkubwa, akiwa amefundisha katika nchi za Tunisia, Algeria na Afrika Kusini, akifanya kazi na klabu mbalimbali zikiwemo El Gawafel Sportives de Gafsa, Stade Gabsien Sports, Averine Sportif de Casserine, na Tunisia ES Metlaoui.

Uzoefu wa kocha huyo unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kwa makipa wa timu hiyo, Djigui Diarra, Aboutwalib Mshery na Khomeiny Abubakar.

Kabla ya kujiunga na Yanga, Mnasria aliwahi kufanya kazi kwa karibu na Folz katika kikosi cha Olympique Akbou kinachoshiriki Ligi Kuu ya Algeria.

Wakiwa Olympique Akbou ambayo msimu uliopita 2024-2025 timu hiyo ilimaliza nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi ya Algeria, Folz alikuwa Mkurugenzi wa Michezo, huku Mnasria kocha wa makipa. Kabla ya hapo, wote walifanya kazi pamoja Lamontville Golden Arrows.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Afrika Kusini, ushirikiano wa Folz na Mnasria ni kama silaha mpya ya Yanga katika vita ya ubingwa wa ndani na mafanikio ya kimataifa.

Uelewano wao nje na ndani ya uwanja ni silaha ambayo inaweza kuwapa Wananchi faida kubwa dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC.

Licha ya kwamba Yanga haijamtambulisha rasmi Kocha Romain Folz ambaye anakuja kuchukua nafasi ya Miloud Hamdi, lakini Mwanaspoti lilishakupa habari kwamba Mfaransa huyo ndiye atakuwa bosi wa benchi la ufundi la timu hiyo kwa msimu ujao.

Kwa mujibu wa Transfermarkt, mtandao unajihusisha na masuala mbalimbali ya soka ikiwemo usajili, Folz anatambulika kuwa Kocha Mkuu wa Yanga tangu Julai 14, 2025.