Dar es Salaam. Kama wewe ni umeathiriwa (uraibu) na tabia ya kujichua basi hili linakuhusu! Wataalamu wa afya wanamezungumzia mbinu mbadala kukabili hali hiyo huku miongoni mwa athari zake ni kupoteza kumbukumbu na kupoteza kiwango kikubwa cha protini mwilini.
Tabia ya baadhi ya wanaume kujichua, jamii imekuwa na dhana kwamba inahusiana moja kwa moja na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume (battery ya kiume), huku ikielezwa kuwa na uwezekano wa kusababisha ugumba.
Akizungumza leo Jumatano, Julai 23, 2024 Daktari kutoka kitengo cha mama na mtoto katika Hospitali ya CCBRT, Justin Nkulu amesema tafiti zinaonyesha hakuna madhara makubwa katika kujichua kwamba inaweza kuathiri nguvu za kiume na uzalishaji kwa mwanaume ikiwa kitendo hicho kitafanywa mara chache.
“Kuna wanaofanya mfululizo hii husababisha mishipa inaweza kulegea na mtu akapata tatizo la upungufu wa nguvu za kiume ila ni mara chache.
“Changamoto kubwa inayoweza kutokea ni ya kisaikolojia, ukishazoea njia mbadala tofauti na njia ya kawaida ambayo Mungu aliiumba, kwa sababu ni lazima ufanye kama umekamilika kiafya, sasa hauwezi kuwa mwanaume na ukawa mwanamke,” amesema.
Amesema kisaijkolojia mtu akishazoea kitendo hicho hamu ya kutamani kuwa na mwanamke huwa inapotea taratibu, anaona anajitosheleza ni kama dawa za kulevya anakuwa mraibu, hata akiwa na mwanamke atarudi kufanya hivyo akiona hajaridhika.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wanasansi wa masuala ya fiziolojia ya homoni wa nchini Marekani akiwemo Dk Michael Reece, umebainisha kwamba;
“Iwapo utakuwa unapenda kujichua hautaona kama unapata ladha yoyote ya tendo la ndoa. Hali hiyo ikizoeleka husababisha kuathiri akili yako na mbaya zaidi unajikuta umekuwa mtumwa wa kitendo hicho.”
Baadhi ya wanaume wamesema walijifunza tabia hiyo walipokuwa na umri mdogo ‘wavulana’ na hivyo kuona ndiyo suluhisho kwao.
“Nilikuwa ninaogopa kuzungumza na wanawake, ilinichukua muda kuja kuoa nadhani kutokana na hii tabia,” amesema Japhet John mkazi wa Sinza.
Mwanaume mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema aliwahi kupitia hali hiyo ambayo ilisababishwa na kuogopa kumpa mimba msichana na suala la kujilinda na maradhi.
Hata hivyo, Dk Nkulu amesema tabia hiyo humpotezea uwezo mwanaume kumkabili mwanamke na inaweza kumuathiri katika nguvu za kiume na uzalishaji baadaye.
Amesema vijana wengi wanafanya kwa sababu ya ushawishi kutoka kwa marafiki, kutokujiamini, kujinyanyapaa, kujiona sifai kupendwa, hali ya kiuchumi kuhisi hataweza kumhudumia mwanamke.
Ili kuondokana na hali hiyo, Dk Nkulu amesema siyo vyema kujiingiza katika mahusiano ya mapenzi ikiwa umri haujafikia.
“Mwili ukidai kuna namna ya kuuzuia, kama uko peke yako tafuta mtu wa kukaa naye na kuzungumza, fanya mazoezi, tafuta kitabu soma, ingia mtandaoni soma vitu vya msingi na ukishindwa vyote tafuta filamu iangalie zenye mafunzo ya kujenga.
“Ukisikiliza muziki au ukifanya kitu kingine itakuondolea ile hali ya matamanio na kama umri unakuruhusu na hali ya kiuchumi basi oa, vitabu vya dini vinasema ili kukwepa zinaa basi oa,” ameshauri Dk Nkulu.
Hata hivyo kwa upande wa wanawake, sayansi inasema kitendo hicho kina madhara kiafya kwao kama ilivyo kwa wanaume, huku wao wakiathirika zaidi kisaikolojia.
– Hukufanya uwe dhaifu, inapoteza protini na kalsiamu mwilini.
– Huleta matatizo kwenye neva nyurolojia ndani ya mwili na kusababisha uoni hafifu
– Upungufu wa nguvu za kiume
– Kupata uraibu (addiction)
– Kupata mfadhaiko wa akili
– Huleta matatizo ya kisaikolojia
– Kutegemea taswira ya mtu asiyekuwepo, picha chafu
– Kufanya makutano haramu, picha na majarida
– Inapunguza wingi wa mbegu (kusababisha ugumba)
– Unalichukia tendo baada ya kumaliza
– Husababisha ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu, ni vigumu kuwa na akili ya utulivu
– Inaongeza aibu na kupunguza uwezo wa kujiamini
– Utapoteza hamu ya kushiriki tendo la ndoa