Mahakama yabariki shehena ya kilo 2,167 za dawa za kulevya kuteketezwa

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemruhusu Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya nchini (DCEA), kuteketeza shehena ya dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa kilo 2167.29.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Julai 23, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Ushindi Swallo, baada kukubaliana na maombi ya Serikali yaliyowasilishwa mahakamani hapo.

Serikali iliwasilisha maombi hayo kwa hati ya dharura ikiomba Mahakama hiyo iridhie dawa hizo ziteketezwe kutokana na  kuwa katika hatari kubwa ya kubadilika mwonekano wake wa asili na wa kikemikali, hivyo wanaomba mahakama hiyo ikubaliane na maombi hayo ya kuteketeza kielelezo hicho (dawa) kabla hazijaleta athari.

Mshtakiwa Najim Mohamed(aliyevaa barakoa) akiwa na Juma Abbas, ambao wanadaia kusafiridha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kilo 882.71 na Methamphetamine zenye uzito wa kilo 2167.29, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi yao ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa maombi ya kuteketeza dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa kilo 2167.29. Picha na Hadija Jumanne

Maombi hayo yanatokana na kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2023 yenye mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya, yanayomkabili mfanyabiashara Najim Mohamed (52) na mke wake, Maryam Mohamed (51) pamoja na mfanyakazi wa ndani wa kiume, Juma Abbas (34).

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili katika mahakama hiyo ambayo ni kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 882.71 pamoja dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa kilo 2,167.29.

Hata hivyo, kesi hiyo ipo katika hatua ya kutajwa mahakamani hapo na upelelezi wake bado haujakamilika.

Hakimu Swallo baada ya kusikiliza maombi ya upande wa mashtaka na majibu ya upande wa utetezi, amesema mahakama hiyo inakubaliana na maombi yote matatu ya upande wa mashtaka iliyowasilisha mahakamani hapo, hivyo inaruhusu kamishna wa DCEA kuteketezwa dawa hizo.

Awali, jopo la mawakili watatu waandamizi wa Serikali, likiongozwa na Frank Nchanila, Foibe Magini na Batilda Mushi, walidai kuwa Juni 10, 2025 waliwasilisha maombi matatu mahakamani hapo, ikiwemo mahakama hiyo iridhie uteketezaji wa dawa hizo.

Alidai maombi hayo yamewasilishwa chini ya kifungu 36(3)(4)(5) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

“Maombi haya tumeyaleta kwa hati ya dharura na yameambatanishwa na kiapo cha Mkaguzi wa Polisi, Pascal Daudi kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini,” amedai wakili Nchanila.

Wakili Nchanila amedai katika maombi hayo wanaomba vitu vitatu ambavyo ni moja, mahakama hiyo ipitie mchanganuo wa dawa hizo na kujiridhisha kama kiapo cha Daudi kinavyoeleza.

“Pili, tunaomba mahakama hii ikubali kielelezo hiki( kilo 2167.29) za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zipigwe picha mbele yako (hakimu) ili  uweze kuthibitisha kwa kujiridhisha na kisha kusaini hati kwa kufuata utaratibu uliopo, ili picha hizo ziweze kuja kuwa sehemu ya kielelezo katika kesi hii,” alisema.

Aliendelea kudai ombi la tatu, wanaiomba mahakama hiyo imruhusu

Kamishna wa DCEA kuendelea na taratibu za kuteketeza dawa hizo aina ya Methamphetamine kwa kuwa ni hatarishi na zina asili ya kubadilika mwonekano wake na kemikali zilizopo pamoja na aina ya utunzaji wake hadi kuja kutumika katika usikilizwaji wa kesi hiyo.

Hata hivyo, wakili wa utetezi Ashirafu Muhidini alipinga maombi hayo yasikubaliwe kutokana na kukiuka sheria.

“Mheshimiwa Hakimu, tunapinga maombi yao yote waliyowasilisha mahakamani hapa kwani yamekiuka sheria ya DCEA,” alidai.

Muhidin alidai wateja wake walikamatwa Desemba 14, 2024 na kielelezo hicho kilifanyiwa uchunguzi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kutolewa majibu Agosti 20,2024 lakini baada ya majibu hayo, Serikali haikuona haja ya kuwasilisha maombi ya kuteketeza kielelezo hicho na kukaa muda mrefu hadi Juni 2025, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za DCEA.

Hata hivyo, hakimu Swallo alitupilia mbali ombi la upande wa utetezi na kukubaliana na maombi ya upande wa mashtaka.

Mshtakiwa, Maryam Mohamed, ambaye ni mke wa Najim, akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi kusafiisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kilo 882.71 na Methamphetamine kilo 2167.29 inayomkabili yeye na wenzake ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa maombi ya Serikali ya kuteketeza kielelezo( Methamphetamine kilo 2167.29). Picha na Hadija Jumanne

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Desemba 15, 2023 katika eneo la Kibugumo Shule lililopo wilaya ya Kigamboni, walisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kilo 882.71.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa kilo 2167.29.