Majaliwa Akutana Na Waziri Mkuu Wa Belarus – Global Publishers

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa alivyopokelewa na Waziri Mkuu wa Belarus

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Belarus, Alexander Turchin na kujadiliana naye masuala ya uwekezaji, biashara, nishati, madini, elimu, afya, teknolojia na kilimo kwenye kikao kilichofanyika leo (Jumanne, Julai 22, 2025) ofisini kwa mwenyeji wake, mtaa wa Sovetskaya, jijini Minsk.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alimweleza mwenyeji wake kuwa, mbali na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia anataraji kuwa ziara hiyo itaongeza chachu ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji, elimu, afya na upatikanaji wa zana za kisasa kwenye kilimo kutokana na fursa mbalimbali zilizoko nchini.

Alisema mazungumzo yao yamefungua milango ya kuimarisha uwekezaji, fursa za biashara na masomo katika vyuo vya elimu ya juu, na kwamba wamekubaliana na mwenyeji wake kuwa Mawaziri wake na Naibu Makatibu Wakuu walioko kwenye ziara hiyo wakutane ili kuanza majadiliano rasmi ya kufanikisha nia ya kampuni ya Minsk Tractor Plant OJSC ya kuleta kiwanda kama hicho nchini.
Aliwaeleza baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wanaotoka Chama cha Wafanyabiashara cha Belarus kwamba hivi sasa Tanzania imepunguza muda wa kupata leseni, imeongeza maeneo ya uwekezaji (TISEZA) na imeboresha sheria za kikodi ili kuhamasisha uwekezaji nchini.

Aliwaeleza fursa nyingine za kuwekeza Tanzania ni uwepo wake kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya kikanda ya SADC na Eneo Huru la Biashara barani Afrika (ACfTA) pamoja na uwepo wa nchi sita zinazoizunguka Tanzania na hazina bandari (land-locked countries) ambazo zina wakazi wengi.

Katika kikao hicho, Mawaziri Wakuu wote wawili walishuhudia utiaji saini wa hati tatu za makubaliano na maktaba mmoja baina ya mawaziri wa nchi hizo mbili. Hati hizo zilizosainiwa leo zinahusu mashauriano ya kisiasa; makubaliano ya kuendeleza sekta ya kilimo na sekta ya elimu.

Aidha, mkataba uliosainiwa leo ni baina ya Chama cha Wafabiashara, Viwanda na Kilimo ya Tanzania (TCCIA) na Chama cha Wafabiashara wa Belarus unaolenga kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Belarus, Alexander Turchin alimshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kufanya ziara ya Kiserikali nchini humo na kuipa heshima nchi hiyo kupokea kiongozi mkuu kutoka Tanzania kwa mara ya kwanza.

Alisema Belarus inaiona Tanzania kuwa mdau muhimu wa ushurikiano katika nyanja mbalimbali na hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo inao utaalamu (expertise) katika nyanja nyingi ambazo zimegusiwa wakati wa majadiliano yao. “Tuko tayari kutoa ushirikiano kwenye maeneo uliyoyataja na wala sioni haya kusema hivyo kwa sababu nchi yetu inao utaalamu mkubwa kwenye maeneo uliyoyaainisha,” alisema.
Alisema mazungumzo yaliyofanyika leo baina ya viongozi hao wakuu ni mwanzo wa ushirikiano wa kudumu ambao utasaidia kukamilisha masuala yaliyoibuliwa kutokana na ziara hiyo. “Ziara hii ni fupi na hatuwezi kukamilisha kila jambo, lakini maeneo yote ya usalama wa chakula, utoaji wa huduma za tiba, kilimo na elimu yanaweza kukamilishwa na timu zetu,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kumtakia heri Mheshimiwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Mapema asubuhi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea kiwanda cha kutengeneza dawa cha Republican Unitary Production Enterprise “Belmedpreparaty” na kiwanda cha kutengeneza matrekta na zana za kilimo cha Minsk Tractor Plant OJSC.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Bw. Shariff Ali Sharriff, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu Wizaya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu pamoja Naibu Katibu Mkuu Kilimo, Dkt. Stephen Nindi.